Kiongozi wa Mapinduzi: Hatufurutu mpaka katika kuyatazama mazungumzo ya Oman kwa jicho zuri au baya
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, ufuatiliaji ndicho kiungo kinachokosekana katika kufanikisha malengo ya nchi na akasisitiza kuwa ajenda ya pamoja ya mihimili mitatu ya dola ni kufanya jitihada za kufanikisha kaulimbiu ya mwaka huu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameyaelezea mazungumzo ya Oman kuwa ni moja ya makumi ya majukumu yanayotekelezwa na Wizara ya Mambo ya Nje na kusisitiza kuwa: masuala ya nchi yasifungamanishwe na mazungumzo hayo, na kosa lililofanywa katika JCPOA, la kufungamanisha masuala yote ya nchi na upigaji hatua wa mazungumzo hayo, halipasi kurudiwa tena.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya kuendelea shughuli za nchi katika nyanja zote za kiviwanda, kiuchumi, za ujenzi, za kiutamaduni na za utekelezaji wa miradi mikubwa na akasema: "hakuna hata moja kati ya masuala haya ambalo lina uhusiano wowote ule na mazungumzo ya Oman".

Sambamba na kuhadharisha juu ya "kufurutu mpaka katika kujenga matumaini au kupoteza matumaini" kuhusiana na matokeo ya mazungumzo hayo, Ayatullah Khamenei ameongezea kwa kusema: " katika hatua za kwanza imefanyika kazi nzuri kuhusu uamuzi wa nchi wa kufanya mazungumzo. Baada ya hatua hii pia inapasa zichukuliwe hatua kwa umakini, ikizingatiwa kuwa mistari myekundu ya upande wetu na ya upande wa pili inajulikana wazi".
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "mazungumzo yanaweza kuwa na tija au yasiwe na tija. Na sisi pia hatuna mtazamo chanya wa kupita kiasi wala mtazamo hasi wa kupita kiasi kuhusu mazungumzo haya. Bila shaka, tuna mtazamo hasi wa kupita kiasi kwa upande wa pili (wa mazungumzo), lakini tuna mtazamo chanya kwa uwezo wetu wenyewe".
Kwa kumalizia hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameashiria jinai zisizo na kifani za genge la utendaji jinai la Kizayuni za kuwashambulia kwa makusudi wagonjwa, waandishi wa habari, magari ya kubebea wagonjwa, hospitali na watoto na wanawake madhulumu wa Ghaza na akasema: kutenda jinai kama hizo kunahitaji kuwa na ukatili na ushenzi usio wa kawaida, sifa ambazo genge hilo la utawala ghasibu limepambika nazo.
Aidha, amesema kuwepo harakati iliyoratibiwa kwa pamoja na Ulimwengu wa Kiislamu katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na ikibidi za kioperesheni ni hitajio lenye uzito mkubwa na akaongeza kuwa: Bila shaka Mwenyezi Mungu atashusha mjeledi wake juu ya madhalimu hao, lakini hilo halipunguzi majukumu mazito ziliyonayo serikali na wananchi.../