Wazayuni waendeleza mashambulizi Ukingo wa Magharibi, wamjeruhi mtoto Mpalestina
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameendeleza mashambulizi na hujuma zao za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi na kumjeruhi kwa risasi mtoto wa kike wa Kipalestina.
Jana usiku wanajeshi wa utawala haramu wa Israel waliwafyatulia risasi Wapalestina katika kitongoji cha Qabatiya kusini mwa mji wa Jenin na kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi na kumjeruhi mtoto mmoja wa kike.
Duru za habari za Palestina zimetangaza kuwa, wanajeshi wa Israel walimfyatulia risasi raia mmoja wa Kipalestina akiwa ndani ya gari na kumjeruhi shingoni na usoni. Mpalestina huyo amelazwa hospitali.
Wanajeshi hao wa Israel pia wameyashambulia maeneo kadhaa upande wa mashariki wa eneo la Tulkarem na kuwatia nguvuni vijaa kadhaa wa Kipalestina.
Duru za Wapalestina pia zimeripoti shambulio la wanajeshi wa Israel mashariki mwa mji wa Nablus katika Ukingo wa Magharibi.
Juzi Jumatatu pia, Kamati ya Wananchi katika kambi ya wakimbizi ya Jenini, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, ilitangaza kuwa hali ya maisha ya wakimbizi ndani ya kambi hiyo inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku na huduma za misaada zimefikia kiwango cha chini sana.