Iran: Urutubishaji urani 'haujadiliki', mazungumzo chini ya mashinikizo hayatakuwa na tija
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema urutubishaji wa madini ya urani ukiwa ni sehemu ya mpango wa amani wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu "haujadiliki" na kwamba mazungumzo ya Tehran na Washington hayatazaa matunda ikiwa yatafanyika kwa mashinikizo na bila ya pande mbil kuheshimiana.
Abbas Araghchi ameyasema hayo leo pembeni ya kikao cha kila wiki cha baraza la mawaziri hapa mjini Tehran, baada ya Mjumbe Maalumu wa Marekani Steve Witkoff kusema Tehran "lazima isimamishe na kuupangua kikamilifu" mpango wake wa kurutubisha urani kwa ajili ya masuala ya nyuklia ili kufikia makubaliano na Washington.
Matamshi hayo yametolewa wakati Araghchi na Witkoff wanatarajiwa kukutana tena nchini Oman siku ya Jumamosi, wiki moja baada ya kufanyika mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya pande hizo mbili tangu Rais wa Marekani Donald Trump ajitoe katika makubaliano ya kihistoria ya nyuklia na Iran mwaka 2018.
"Mpango wa urutubishaji urani wa Iran ni suala la uhakika na la dhati na tuko tayari kutoa hakikisho la kuwepo na imani juu ya masuala yanayotiliwa wasiwasi, lakini suala la urutubishaji urani halijadiliki," amesisitiza Araghchi mbele ya waandishi wa habari.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria kuendelea kile kinachoitwa kampeni ya mashinikizo ya Marekani dhidi ya Iran wakati wa mazungumzo hayo, na akasema: "msimamo wetu na vitendo vyetu viko wazi, hawataweza kufikia chochote kupitia mashinikizo. Ikiwa mazungumzo hayo yataegemezwa katika misingi ya usawa na yakifanyika katika mazingira ya heshima, yanaweza kuendelea, lakini hakuna kitakachopatikana kwa mashinikizo na kulazimisha misimamo yao; na tumethibitisha hilo kwa misimamo yetu na vitendo vyetu. Tutashiriki katika mazungumzo kwa utulivu kamili bila kuathiriwa na mashinikizo au mkondo wowote".
Araghchi amelaumu pia "misimamo inayogongana na inayokinzana" inayotoka kwenye serikali ya Trump kabla ya mazungumzo ya Jumamosi.
"Kama nilivyoeleza, katika kipindi hiki tumesikia misimamo inayogongana na inayokinzana, na Bw. Witkoff amezungumza kwa namna kadhaa hadi sasa; misimamo halisi itafafanuliwa kwenye meza ya mazungumzo," amesisitiza mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran.../