Iran yaikosoa Marekani kwa kuibua masharti mapya ya kuondoa vikwazo
(last modified Mon, 11 Apr 2022 02:36:29 GMT )
Apr 11, 2022 02:36 UTC
  • Iran yaikosoa Marekani kwa kuibua masharti mapya ya kuondoa vikwazo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani imeibua masharti mapya inayotaka Tehran itekeleze ili iondolewe vikwazo sanjari na kuhuishwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015.

Kwa mujibu wa televisheni ya Press TV, Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Jumapili na kusisitiza kuwa, Iran kamwe haiwezi kukiuka mistari yake miyekundu kwa kutii masharti hayo mapya ya Marekani.

Amesema Iran itaendelea kufanya juu chini kuhakikisha kuwa makubaliano yanayofikiwa katika mazungumzo ya Vienna ya kundolewa vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ni thabiti na ya kudumu.

Amir-Abdollahian ameeleza bayana kuwa: "Kuhusu suala la kuondoa vikwazo, wao (Wamarekani) wanashupalia tu kuibua masharti mapya ambayo yako nje ya mazungumzo."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa, Tehran inataka kuondolewa vikwazo, lakini jambo hilo linapaswa kufanyika kwa njia ya heshima, na kupitia makubaliano yenye nguvu na ya kudumu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, "Tunakaribia kuhitimisha majadiliano ya kiufundi na nchi tatu za Ulaya, lakini tunakabiliwa na mgogoro wa vita Ukraine. Tehran haitaki mkopo au pesa zozote kutoka Marekani, lakini inataka kuachiwa fedha na mali zake."