Mkuu wa Kamati ya Bunge ya Usalama wa Taifa Iran ajibu vitisho vya Waziri wa Ulinzi wa Marekani
(last modified Fri, 02 May 2025 07:39:20 GMT )
May 02, 2025 07:39 UTC
  • Ebrahim Azizi
    Ebrahim Azizi

Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu amejibu vitisho vya Waziri wa Ulinzi wa Marekani akisema kuwa, Wamarekani wenyewe ndio watakaolipa gharama ya mienendo yao inayokinzana.

Ebrahim Azizi ameandika kwenye akaunti yake ya X akijibu vitisho vya Waziri wa Ulinzi wa Marekani na mienendo inayopingana ya nchi hiyyo (mazungumzo na vitisho) kwamba: "Iwapo, sambamba na maungumzo ya sasa, vitisho vyako vitasababisha hatua inayokwenda kinyume na maslahi ya kitaifa na usalama wa Iran ya Kiislamu, ni nyinyi mtakaolipa gharama kwa wakati na mahali tutakapoainisha sisi."

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alichapisha ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X ambao ulikuwa na vitisho vya kijeshi badala ya kuheshimu sheria na kaida za mazungumzo.

Hegseth, akihutubia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ameandika: “Tunaona uungaji mkono wenu mbaya sana kwa Wahouthi... Mtagharamia msaada huu kwa wakati na mahali tutakapochagua.”

Matamshi hayo ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani, katika kuelekea kwenye duru ya nne ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani, ni hatua iliyokwenda kinyume na kaida za kidiplomasia. Wachambuzi wengi wanaamini hatua hiyo ni ishara ya mgogoro katika siasa za Marekani na kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na hali halisi mpya ya kanda ya Magharibi mwa Asia.