Iran: Tutajibu chokochoko yoyote ya kijeshi ya Marekanii au Israel
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, hatua zozote za kijeshi za Marekani au utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mamlaka ya kujitawala na maslahi ya taifa ya Iran zitapatiwa jibu la haraka na mwafaka.
Amir Saeed Iravani amesema hayo katika barua yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuonya vikali juu ya chokochoko ya kijeshi ya Marekani au utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amir Saeed Iravani, balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ametoa radiamali kwa vitisho vya hivi karibuni vya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegthes katika barua yake kwa Baraza la Usalama na kuzitaja tuhuma zao kuwa hazina msingi na ni za uchochezi.
Amesisitiza kuwa Marekani na Israel zitabeba dhima ya uvamizi wowote. Katika barua hiyo, Iran imesema kwa uwazi kwamba, chokochokko yoyote ya kijeshi itakabiliwa na jibu la haraka na mwafaka, na kwamba dhima ya yatakayotokana na hatua hizo yatakuwa kwa Marekani na utawala wa Kizayuni.
Iran inakanusha shutuma na vitisho vyovyote kutoka Israel na Marekani na inavichukulia kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Aidha Iran imelitaka Baraza la Usalama lichukue hatua ya kulaani vitisho hivyo na kukomesha uchokozi wa kijeshi.
Barua hii inaakisi msimamo thabiti wa Iran dhidi ya vitisho vya nje na msisitizo wake juu ya haki ya kutetea mamlaka yake ya kujitawala na umoja wa ardhi yake.