Iran yakaribisha upatanishi wa Oman uliopelekea US kusitisha mashambulizi dhidi ya Yemen
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei amekaribisha taarifa ya Oman kuhusu kusitishwa kwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Yemen, akisema kuwa nchi za eneo hili hazitasahau Muqawama wa watu wa Yemen dhidi ya uvamizi wa kigeni.
Katika taarifa jana Jumatano, Baqaei amesifu uthabiti wa taifa la Yemen katika kuwaunga mkono Wapalestina huku kukiwa na mauaji ya kimbari na uvamizi wa Israel, pamoja na kusimama kwao kidete dhidi ya hujuma za mara kwa mara za Marekani dhidi yao.
Huku akishukuru juhudi za serikali ya Oman katika kupatanisha usitishaji mapigano kati ya Washington na Sana’a, Baqaei ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti kusitisha mashambulizi ya Israel dhidi ya Yemen.
Kadhalika ameishutumu serikali ya Marekani kwa kuhusika na jinai zinazofanywa na utawala wa Israel dhidi ya watu wa Yemen. Hapo awali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr bin Hamad bin Hamood Albusaidi alithibitisha kufikiwa makubaliano ya kusitisha makabiliano kati ya Marekani na Yemen.
"Kufuatia mazungumzo na mawasiliano ya hivi majuzi yaliyofanywa na Utawala wa Kisultani wa Oman na Marekani na mamlaka husika huko Sana'a, Jamhuri ya Yemen, yenye lengo la kupunguza taharuki, makubaliano ya kusitisha mapigano yamefikiwa kati ya pande hizo mbili," Albusaidi amesema katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Marekani na utawala ghasibu wa Israel zimekuwa zikifanya mashambulizi ya anga ya mara kwa mara dhidi ya Yemen katika miezi ya hivi karibuni, yakilenga vituo muhimu nchini humo katika juhudi za kuwazuia Wayemeni kuwaunga mkono Wapalestina. Navyo vikosi vya Wanajeshi wa Yemen vimekuwa vikilenga meli zenye mfungamano na Israel na Marekani katika Bahari Nyekundu na kushambulia maeneo yanayokaliwa na Israel.
Jana Jumatano, Harakati ya Muqawama ya Ansarullah ya Yemen ilisema kuwa, makubaliano ya usitishaji vita na Marekani hazijumuishi operesheni dhidi ya utawala haramu wa Israel.