Sababu ya Iran kutolegeza msimamo kuhusu haki yake ya kurutubisha madini ya urani
(last modified Tue, 20 May 2025 03:49:31 GMT )
May 20, 2025 03:49 UTC
  • Sababu ya Iran kutolegeza msimamo kuhusu haki yake ya kurutubisha madini ya urani

Ikiwa ni katika kujibu matamshi ya Steve Whitkoff, mkuu wa timu ya mazungumzo ya Marekani, Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa: "Kufikiwa makubaliano kunawezekana na tuko tayari kuingia katika mazungumzo mazito. Kwa vyovyote vile, urutubishaji nchini Iran utaendelea tu, makubaliano yafikiwe au la."

Abbas Araghchi ameandika kwenye akaunti yake ya X baada ya matamshi ya Steve Whitkoff, kuhusu ulazima wa kutorutubishwa urani nchini Iran kwamba: "Katika mazungumzo kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, pande za Marekani kimsingi zina uhuru wa kusema lolote wanalotaka hadharani kwa madhumuni ya kupunguza mashinikizo ya makundi yenye ushawishi na wahusika hasimu ambao, kwa uchache walihudumu katika tawala zilizopita na ambao hawataki kuona mapatano yakifikiwa kati ya pande mbili."

Araqchi ameongeza kuwa: "Lakini Iran inawajibika tu kuhusu tabia zake yenyewe, na kwa hivyo, sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuepuka kupayuka hadharani. Hasa kwa kuzingatia nyufa zinazoongezeka kila siku ambazo zinaonekana wazi siku hizi kati ya misimamo inayotangazwa hadharani na ya siri upande wa Marekani, na pia mabadiliko ya kila wiki kwenye misimamo hiyo.

Huku akisisitiza kwamba msimamo wa Iran kuhusu haki zake kama mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) uko wazi kabisa na hauwezi kufasiriwa vingine, Araghchi amebainisha kuwa: "Hakuna hali au mazingira ambayo yatawafanya Wairani wabadilishe msimamo na kupelekea wanyimwe haki hizo. Kudhibiti mfumo mzima wa urutubishaji ni mafanikio ya ndani ambayo yamefikiwa kupitia kazi ngumu ya muda mrefu, mafanikio ambayo ni matokeo ya miaka mingi ya juhudi za kisayansi na kujitolea kukubwa kwa mali na roho."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameandika: "Ikiwa kweli Marekani inataka Iran isiwe na silaha za nyuklia, makubaliano yanaweza kufikiwa kirahisi, na tuko tayari kushiriki katika majadiliano mazito ili kuzuia kabisa hali kama hiyo itokee."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Araqchi 

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani na kusema: "Kufikiwa makubaliano na Marekani ni jambo linalowezekana, lakini utekelezaji wake unahitaji sharti la kimsingi, ambalo ni kwamba upande wa Marekani uepuke kutumia mabavu na kuutwisha upande wa pili matakwa yake. Kwa sababu hatutasalimu amri kwa vyovyote vile."

Steve Whitkoff alikuwa amedai awali kwamba Marekani ilikuwa imewapendekezea Wairani bila kuwadharau kwamba wafikirie suala la kutorutubisha urani kwa hoja kuwa Marekani haiwezi kufikia mapatano ambayo yanairuhusu Iran kurutubisha urani ndani ya nchi na kuwa haitairuhusu kuunda bomu la nyuklia.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikisisitiza juu ya haki yake halali ya kutumia kwa amani nishati ya nyuklia na inafuatilia haki hiyo ndani ya fremu ya mikataba ya kimataifa kama vile NPT na chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.

Kwa mujibu wa sheria za wakala huo, kurutubisha urani kwa ajili ya matumizi ya amani kama vile uzalishaji umeme na matibabu ni haki ya kisheria ya Iran, na hakuna nchi yoyote inayoweza kuipokonya haki hii. Iran imethibitisha kuwa siku zote inazingatia majukumu yake ya kimataifa na kwamba iko tayari kufanya mazungumzo kwa ajili ya kuondolewa vikwazo vya kidhalimu. Kwa hivyo, haioni sababu yoyote ya kufumbia macho haki hiyo, kwani suala hili si tu linahusiana moja kwa moja na usalama wake wa taifa, bali pia linachangia pakubwa maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia ya nchi.

Licha ya vikwazo na kujitoa kwa upande mmoja Marekani katika mapatano ya JCPOA, lakini bado Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kimataifa na pia kushirikiana kikamilifu na wakala wa IAEA. Katika duru nne za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani, timu ya mazungumzo ya Iran pia imesisitiza kwa nia njema juu ya matakwa halali ya Iran ya kutumia kwa amani nishati ya nyuklia.

Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yanafanyika katika hali ambayo makundi yenye itikadi kali na yanayochochea vita pamoja na baadhi ya maafisa wa serikali ya Washington wanaendelea kuwa na misimamo mikali ya chuki dhidi ya Iran.

Iran daima imekuwa ikisisitiza kwamba italinda mafanikio yake ya nyuklia, ikiwa ni pamoja na urutubisha wa ndani ya nchi ambao umepatikana kupitia juhudi na kujitolea kukubwa kulikofanywa na wasomi na wanasayanzi wa ndani. Hivyo matamshi na vitisho vya Wamarekani havitaathiri uamuzi huu kwa vyote vyote vile.

Ni wazi kuwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yatazaa matunda pale tu maafisa wa Marekani watakapojiepusha kutoa matamko yasiyofaa na wakati huo huo kuandaa mazingira ya kuondolewa vikwazo vya upande mmoja na vya kidhalimu dhidi ya Iran.