Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yaliyoanza leo mjini Muscat, Oman
(last modified Sat, 12 Apr 2025 09:18:37 GMT )
Apr 12, 2025 09:18 UTC
  • Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yaliyoanza leo mjini Muscat, Oman

Esmail Baqaei Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza kuwa: Ujumbe wa Iran ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Sayyid Abbas Araqchi umeelekea Muscat mji mkuu wa Oman yanakofanyika mazungumzo kati ya Iran na Marekani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametuma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kuhusu safari ya ujumbe wa Iran huko Muscat kwa ajili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na wawakilishi wa serikali ya Marekani na kueleza kwamba: Tumedhamiria kutumia uwezo wote kulinda mamlaka ya Iran na maslahi ya taifa. Mazungumzo kati ya wawakilishi wa Iran na Marekani yatafanyika leo (Jumamosi), Aprili 12, huko Muscat, mji mkuu wa Oman. 

Ujumbe wa Iran katika mazungumzo hayo umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Sayyid Abbas Araqchi. Steven Witkoff, Mjumbe Maalumu wa Rais Donald Trump katika Masuala ya Mashariki ya Kati ameongoza timu ya Marekani katika mazungumzo hayo na Iran huko Oman. 

Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika siku za karibuni walitangaza misimamo yao kuhusu mazungumzo hayo tajwa. Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kwamba: "Iran na Marekani Jumamosi zitakuwa na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja huko Oman katika ngazi ya viongozi wa ngazi ya juu. Hii ni fursa na wakati huo huo ni mtihani. Mpira upo katika uwanja wa Marekani."

Majid Takht-Ravanchi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayeshughulikia Masuala ya Kisiasa ameashiria muelekeo wa serikali kuhusu kadhia ya nyuklia na kusema: Jamhuri ya Kiislamu kama ilivyokuwa huko nyuma na kwa kufuata sera ya maelewano iko tayari kufanya mazungumzo kuhusu miradi yake ya nyuklia yenye malengo ya amani. 

Majid Takht-Ravanchi 

Takht-Ravanchi ameashiria mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja katika kadhia ya nyuklia kati ya Iran na Marekani huko Muscat, mji mku wa Oman na kusema: Kuna fursa nzuri ya kufikia makubaliano ikiwa upande wa Marekani hautaibua masuala na matakwa yasiyo na uhusiano na ikaweka kando vitisho na lugha ya kibabe. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini katika kufanya mazungumzo na kufikia maelewano chini ya kivuli cha ushirikiano wa pande mbili; na kwa mtazamo wa Iran, ubabe na utumiaji mabavu wa aina yoyote haukubaliki.

Mazungumzo yasiyo ya moja na Marekani kwa ajili ya kufufua makubaliano ya JCPOA yalifanyika pia katika miaka ya karibuni, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikulipa kisogo suala hilo. Hata hivyo kilichokwamisha kufikia natija mazungumzo hayo ni msimamo wa Marekani wa kutaka kuirubuni kimabavu Iran na kuibua mambo yasiyohusiana na mazungumzo hayo. Sababu ya mazungumzo ya Oman kutokuwa ya moja kwa moja imetokana pia na kutokuwa na imani na Marekani, kulikosababishwa na nchi hiyo kutotekeleza ahadi zake katika mazungumzo ya ana kwa ana ya JCPOA.

Mwaka 2018, wakati Rais Donald Trump wa Marekani alipokuwa katika muhula wake wa kwanza wa urais alisaini dikrii ya utekelezaji na kuamua kuiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya JCPOA. Baada ya hapo, vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran ambavyo kwa  mujibu wa ahadi za Marekani ndani ya JCPOA vilipasa kuwekwa kando, vilirejeshwa na kutekelezwa tena dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Mwaka 2018- Trump alipoiondoa Marekani katika JCPOA 

Katika miaka ya karibuni pia, maafisa wa Marekani wameiwekea Iran vikwazo vya upande mmoja bila kujali makubaliano ya JCPOA na maazimio ya Umoja wa Mataifa. Ukweli ni kuwa, matokeo muhimu zaidi ya mazungumzo hayo yalipasa yawe ni  kuondolewa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani, ambavyo vimekuwa vikirefushwa kila mara na White House kwa kushirikiana na waitifaki wake wa Ulaya. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza siku zote kwamba mazungumzo itakayofanya yatahusu kadhia ya nyuklia pekee na kwa lengo la kuondolewa vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa. Miradi ya nyuklia ya Iran katika miaka ya karibuni imekuwa ikisimamiwa na kukaguliwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ambapo ripoti na wakaguzi wa  wakala huo wamethibitisha kuwa miradi hiyo inafanyika kwa malengo ya kiraia. 

Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya huko Oman nayo pia yanafanyika kwa lengo la kuondolewa vikwazo na kuiwezesha Iran kunufaika kiuchumi. Licha ya kuwepo shaka kubwa kuhusu nia ya Marekani ya kufikia makubaliano, Iran inatumia fursa hiyo kubainisha msimamo wake thabiti kuhusu utumiaji wa nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani; na katika mazungumzo ya Oman, itapimwa na kutathminiwa tena irada na nia ya Marekani ya kutatua tatizo hilo na kuiondolea vikwazo Iran.