Kharrazi: Dunia ya kambi moja imeyoyoma, kuna haja ya mazungumzo ya kikanda
(last modified Wed, 21 May 2025 07:33:08 GMT )
May 21, 2025 07:33 UTC
  • Kharrazi: Dunia ya kambi moja imeyoyoma, kuna haja ya mazungumzo ya kikanda

Mkuu wa Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Iran amesisitiza kuwa mfumo wa kambi moja umeyoyoma na sasa kumeibuka madola yenye nguvu ya kikanda na kusema: "Suluhisho pekee la changamoto za Mashariki ya Kati ni mazungumzo ya moja kwa moja kati ya nchi za eneo hilo bila ya uingiliaji wa madola ya nje ya kanda hiyo."

Sayyid Kamal Kharrazi amesema katika kikao maalumu cha Jukwaa la Mazungumzo la Tehran kwamba, hali nzuri inayoshuhudiwa hivi sasa katika uhusiano wa Iran na majirani zake ni kielelezo cha athari nzuri za mazungumzo.

Akisisitiza kwamba nchi mbalimbali zinapaswa kuwa na nafasi kubwa zaidi katika mfumo wa kimataifa kwa kuegemea kwenye sera ya dunia ya kambi kadhaa, Kharrazi amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, pamoja na diplomasia yake amilifu, ni kigezo chenye mafanikio cha ushirikiano wa kieneo."

Mkuu wa Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Iran ameongeza kuwa: "Kuporomoka kwa ubeberu wa Marekani ni fursa ya kupata uhusiano wenye usawa zaidi, na madola kama vile China, India, Russia na Iran yanaunda mfumo mpya."

Kharrazi aidha ameeleza kuwa, utiifu wa Ulaya kwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel umezuia nchi hizo kuwa na uhusiano na Iran na kuongeza kuwa: "Utaalamu wa nyuklia wa Iran ni wa ndani ya nchi kikamilifu na hauwezi kutenguliwa, na sharti ya makubaliano yoyote ni kuondolewa vikwazo."