Iran na Oman zatiliana saini hati 18 za mikataba ya ushirikiano
(last modified Wed, 28 May 2025 03:28:13 GMT )
May 28, 2025 03:28 UTC
  • Iran na Oman zatiliana saini hati 18 za mikataba ya ushirikiano

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman zimetiliana saini hati 18 za mikataba ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali.

Katika ziara rasmi ya Dk Masoud Pezeshkian, Rais wa Iran mjini Muscat siku ya Jumanne, hati 18 za ushirikiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman zilitiwa saini mbele ya Sultan Haitham bin Tariq na Rais Pezeshkian.

Nyaraka hizo zitakuwa msingi wa kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili katika nyanja za kisheria, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni, elimu, afya, ulinzi, vyombo vya habari, teknolojia, nishati na madini.

Wakati huo huo, Rais Pezeshkian amesema Tehran inathamini jukumu amilifu na la kujenga la Oman katika mchakato wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya Iran na Marekani na inatumai kuwa yataleta matokeo mazuri.

Daktari Pezeshkian amesema hayo katika mazungumzo yake na Sultani Haitham bin Tariq wa Oman mjini Muscat hapo jana.

Akisisitiza nafasi ya kistratijia ya Oman katika sera ya kigeni ya Iran, Pezeshkian alisema Tehran ina imani kamili na Oman, na uaminifu huu unaweka wajibu wa pamoja kwa pande zote mbili za kuimarisha uhusiano.

Rais Pezeshkian alisema Iran iko tayari kuinua ushirikiano na Oman katika nyanja zote, akiamini kuwa nchi hizo mbili zina uwezo ambao unaweza kutumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kila mmoja na mataifa mengine katika eneo.

"Tuko tayari kufanya chochote kilicho ndani ya uwezo wetu kwa ajili ya hadhi na adhama ya Waislamu. Kila mmoja wetu ana uwezo ambao unaweza kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kila mmoja wao na ya mataifa mengine katika eneo hili," alisema.