Iran yamnyonga jasusi mwingine wa shirika la kijasusi la Mossad la Israel
Idara ya Mahakama ya Iran imeripoti kuwa mtu mmoja aliyekamatwa mwaka 2020 na kutiwa hatiani kwa kushirikiana kwa kiwango kikubwa na shirika la kijasusi la Israe (Mossad), amenyongwa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Idara ya Mahakama, Mizan, “Baada ya kufanyiwa uchunguzi, kukamatwa, na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, Pedram Madani aliyepatikana na hatia ya ujasusi kwa niaba ya utawala wa Kizayuni, alihukumiwa adhabu ya kifo baada ya taratibu zote za kisheria kukamilika, ikiwemo kuidhinishwa kwa hukumu hiyo na Mahakama Kuu ya Iran.”
Ripoti hiyo imeeleza kuwa Madani alikamatwa mjini Tehran mnamo mwaka 2020 kwa hatia ya “kufanya ujasusi kwa niaba ya huduma ya kijasusi ya utawala ghasibu wa Kizayuni (Mossad)” na “kupata utajiri haramu kupitia sarafu za kigeni (euro) na fedha za mtandao (Bitcoin) huko Ulaya.”
Imedokezwa kuwa Madani alikuwa akitoa taarifa za siri na kufanya mikutano na maafisa wa Mossad nje ya nchi. “Mtuhumiwa aliyekuwa akisafiri kwenda na kurudi Ujerumani kabla ya kukamatwa kwake, alipokea mafunzo kutoka Mossad na alijaribu kuajiri watu na kukusanya taarifa za siri kupitia mifumo salama ya mawasiliano."
Aidha, imeelezwa kuwa Madani alikutana na afisa wake wa moja kwa moja wa Mossad kwenye ubalozi wa utawala wa Kizayuni mjini Brussels, katika mojawapo ya mikutano yake mingi nje ya Iran. Pia aliripotiwa kusafiri hadi katika "ardhi zinazokaliwa kwa mabavu" kabla ya kukamatwa mwaka 2020–2021.
“Baada ya kukamilika kwa mchakato wa kesi ya jinai, Pedram Madani alipatikana na hatia ya ujasusi kwa niaba ya Mossad, na mashtaka ya kufanya uharibifu mkubwa katika ardhi na kuasi dhidi ya Mwenyezi Mungu (moharabeh), na akahukumiwa kunyongwa. Hatimaye, baada ya hatua zote za kisheria kukamilika, adhabu hiyo imetekelezwa kwa njia ya kunyongwa.”
Mwezi Aprili, Mahakama ya Iran pia ilitangaza kutekelezwa kwa adhabu ya kifo dhidi ya jasusi mwingine wa Mossad, Mohsen Langarneshin, ambaye alihusishwa na mauaji ya afisa wa IRGC, Kanali Hassan Sayyad Khodaei, mjini Tehran mnamo Mei 22, 2022, kwa kushirikiana na washambuliaji waliokuwa wakitumia pikipiki.
Langarneshin alikiri makosa yake hadharani katika kila hatua ya uchunguzi, mashitaka na kesi yake.