Iran yazindua mpango wa kuzalisha megawati 20,000 za umeme wa nyuklia
(last modified Thu, 29 May 2025 04:35:57 GMT )
May 29, 2025 04:35 UTC
  • Iran yazindua mpango wa kuzalisha megawati 20,000 za umeme wa nyuklia

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema Jamhuri ya Kiislamu imezindua mpango unaolenga kuzalisha hadi megawati 20,000 za umeme kutokana na shughuli zake za amani za nishati ya nyuklia.

Mohammad Eslami ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano uliofanyika katika mji mkuu Tehran kujadili viwango vya tija vya shirika hilo.

"Mradi huu mkubwa kwa hakika umezinduliwa, na kampuni tekelezi zimeundwa ili kuendeleza jitihada hii kwa usaidizi wa serikali," amesema.

Eslami amebainisha kuwa, katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei amekuwa akisisitiza umuhimu wa kufikia lengo hilo. "Na tunafanya kazi kufikia lengo hili," afisa huyo mkuu wa masuala ya nyuklia amesema.

Akizungumza Februari iliyopita, Eslami alisema matarajio hayo yalitarajiwa kutimizwa kufikia mwaka 2041.

Akiongezea kwenye kauli zake, ametoa mfano wa shughuli za nyuklia za Iran zilizofanikiwa, akisema Kinu cha Nyuklia cha Bushehr kilichoko kusini mwa Iran "kimezalisha kilowati-saa bilioni 72 za umeme katika kipindi cha miaka 10 iliyopita."

Hii "imeokoa kiasi kinacholingana na mapipa milioni 110 ya mafuta, huku gharama ya ujenzi wa kituo hicho ikiwa takriban euro bilioni moja," afisa huyo alisema.

Jamhuri ya Kiislamu, ikiwa inaendana na malengo yake makuu, imekuwa ikiendeleza kwa kasi mpango wake wa nishati ya nyuklia, licha ya kukabiliwa na vikwazo haramu na vya upande mmoja kutoka kwa Marekani na washirika wake.

Pia mwaka jana, Eslami alitangaza ujenzi wa kinu kipya cha nyuklia katika jimbo la pwani la kusini mwa Iran la Hormozgan kwa uwekezaji wa dola bilioni 15 za Kimarekani.

Alibainisha wakati huo kuwa mradi wa ujenzi wa Kinu cha Nyuklia cha Iran-Hormoz, ulikuwa "mkubwa zaidi" kuliko kinu cha nyuklia cha Bushehr, kinu chenye uwezo wa kuzalisha megawati 1,000 kilichojengwa na Urusi na kukabidhiwa Septemba 2013 baada ya miaka mingi ya ucheleweshaji.

Huku ikiendeleza azma yake, nchi hiyo pia imeendelea kufanya kazi kwa karibu na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), na kutii majukumu yake chini ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).