Iran yapokea ‘vipengele vya’ mapendekezo ya Marekani kupitia Oman
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amethibitisha kuwa nchi yake imepokea baadhi ya vipengele vya mapendekezo kutoka kwa Marekani, yaliyowasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, ambaye nchi yake inatekeleza jukumu la upatanishi katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington.
Araghchi ametoa taarifa hiyo kupitia chapisho katika ukurasa wake wa X (zamani ukijulikana kama Twitter) siku ya Jumamosi.
"Ndugu yangu Badr Albusaidi, mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, amefanya ziara fupi hapa Tehran leo na kuwasilisha vipengele fulani vya mapendekezo ya Marekani."
Ingawa hakufichua maudhui ya mapendekezo hayo, amesisitiza kuwa jibu la Tehran litazingatia maadili ya kitaifa, uhuru wa taifa na maslahi ya wananchi wa Iran.
Katika tukio jingine Jumamosi jijini Tehran, Araghchi amepinga vikali mashinikizo ya nchi za Magharibi ya kuitaka Jamhuri ya Kiislamu iache kurutubisha madini ya urani, akiyataja mashinikizo hayo kuwa ni juhudi za kulitwisha taifa la Iran matakwa yao.
Araghchi amesema hayo alipofanya ziara katika Haram ya Imam Khomeini (MA), kusini mwa mji mkuu Tehran Jumamosi, ili kujadidisha utiifu wake kwa itikadi za Muasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu.
"Wakati pande nyingine zinaposema lazima tukomeshe urutubishaji, kimsingi zinajaribu kutwisha aina fulani ya utawala na ukuu wake juu yetu," amesema Araghchi.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza kuwa, "Chini ya sheria za kimataifa, tuna haki sawa na nchi nyingine yoyote ile kufaidika na teknolojia ya amani ya nyuklia, ikiwa ni pamoja na kurutubisha (urani)."
Tangu mwezi Aprili, Iran na Marekani zimekuwa katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kupitia uratibu wa Oman, kwa lengo la kutatua masuala ya nyuklia na vikwazo.
Marekani imetoa vitisho mara kadhaa vya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran, na pia imesisitiza kupunguzwa kwa kiwango cha urutubishaji wa urani hadi "sifuri."
Hata hivyo, Tehran imeendelea kushikilia kuwa kutambuliwa kwa haki yake ya nyuklia pamoja na kuondolewa kwa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani ni masuala yasiyo na nafasi ya mazungumzo.
Araghchi ameongeza kuwa Tehran inasalia imara katika dhamira yake ya kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani, ambapo ameashiria fatwa ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, inayokataza vikali utengenezaji wa silaha za nyuklia.