Wimbi jipya la makombora ya Iran lawawafanya walowezi wa Kizayuni kurudi tena mashimoni
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) limefanya wimbi jipya la mashambulio ya makombora yakiwa ni mashambulizi ya nane tangu Ijumaa - dhidi ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ikiwa ni sehemu ya "Operesheni ya Ahadi ya Kweli III."
Takriban saa 11 kasoro dakika 10 za alfajiri ya leo Jumatatu kwa majira ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, mamia ya makombora yamevurumishwa kutoka Iran kuelekea maeneo ya kimkakati na nyeti huko Tel Aviv na Haifa.
Operesheni ya kulipiza kisasi ya Iran, ilianza siku ya Ijumaa chini ya kaulimbiu ya "Ya Ali ibn Abi Talib," kutokana na kwenda sambamba na maadhimisho ya sikukuu ya Ghadir.
Ving'ora vimesikika katika maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni huku maafisa wa Israel wakiwaamuru walowezi wa Kizayuni kukimbilia haraka katika mashimo ya chini ya ardhi. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Israel.
Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zimenasa makombora ya Iran yakivunja safu nyingi za mifumo ya ulinzi wa anga ya Israel na kupiga shabaha zilizokukusudiwa kwa ustadi mkubwa.
Miongoni mwa maeneo Israel yaliyoathiriwa vibaya ni kituo cha kuzalisha umeme cha Haifa. Video zinaonesha kinateketea kwa moto kufuatia shambulio la makombora la Iran.
Kituo cha kuzalisha umeme cha Haifa kiko kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na ni sehemu muhimu ya miundombinu ya nishati ya utawala wa Kizayuni na kimekuwa chini ya mfululizo wa mashambulizi tangu Oktoba 7, 2023.
Vyombo vya habari vya Israel vimetangaza kuwa kituo hicho kinacholindwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa Arrow 3, kimeharibiwa na shambulio la makombora la Iran lakini jeshi la utawala wa Kizayuni limepiga marufuku kupiga picha na kuchukua video za maeneo ambayo yanasambaratishwa na makombora ya Iran.