Araqchi: Mazungumzo ya kuhitimisha mpango wa nyuklia wa Iran hayakubaliki
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza kuwa, ikiwa lengo la mazungumzo ni kuhitimisha mpango wa nyuklia wa Iran, jukumu na ushiriki wa Ulaya na Uingereza katika mchakato wa mazungumzo hayo litakuwa batili na hilo halina maana yoyote.
Abbas Araqchi amesema hayo katika majibu yake kwa Kaja Kallas, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya na kusisitiza msimamo wa Iran ni kupinga mazungumzo yoyote yale ambayo lengo lake ni kutaka kuifanya Iran iachane na mpango wa nyuklia wenye malengo ya amani.
Matamshi haya yanaashiria kuongezeka mvutano kati ya Iran na Umoja wa Ulaya kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na hilo linaweza kuathiri mchakato wa mazungumzo yajayo. Iran imesema wazi kwamba mazungumzo yoyote lazima yaheshimu haki za nyuklia za nchi hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Iwapo mratibu wa JCPOA anaamini kwamba lengo la mazungumzo yoyote tarajiwa ni kusitisha mpango wa nyuklia wa Iran, hii ina maana ya kupuuza haki zetu chini ya NPT."
Matamshi haya sio tu kwamba yanaonyesha msimamo thabiti wa Iran dhidi ya mashinikizo ya kimataifa, lakini pia yanaweza kuonekana kama onyo kwa nchi za Magharibi kwamba jaribio lolote la kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran litakabiliwa na upinzani mkali.
Iran inataka kuhifadhi haki zake za teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani na haiko tayari kubadilisha msimamo huo hata kwa kushinikizwa.