Qalibaf: Mauaji ya kimfumo ya Wapalestina huko Gaza yanakumbusha jinai za Wanazi
Mohammad Baqer Qalibaf Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amelaani mauaji ya kimfumo ya Wapaletsina yanayotekelezwa na utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kuyataja kuwa yanakumbusha jinai zilizofanywa na Wanazi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Qalibaf ameeleza haya kupitia hotuba aliyoitoa jana katika Mkutano wa Sita wa Maspika wa Mabunge Duniani katika mji wa Geneva, Uswisi.
Spika wa Bunge la Iran amesema: Wabunge wa ngazi za juu kutoka maeneo yote ya dunia wamekutana katika mkutano huo ulioanza shughuli zake jana Julai 29 hadi 31 katika ukumbi wa Palais des Nations, ili kutilia mkazo suala la udumishaji haki mkabala wa wimbi la ukandamizaji linalowasukuma wanadamu kuelekea shimoni.
Amesema, maafa yanajiri Gaza, ambayo hayana kifani; na yanaweza tu kulinganishwa na kurasa za giza zaidi za historia ya mwanadamu.
"Tunashuhudia kuibuka kwa Wanazi wa karne ya 21. Utawala wa Kizayuni unatekeleza uhalifu wa kutisha zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia,”
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, Wazayuni, ambao ni sawa na Wanazi wa karne ya 21 wanapaswa kukomeshwa kabla ya ubinadamu kuzama daima katika dhoruba ya ukandamizaji.