Iran yamnyonga gaidi wa kitakfiri wa Daesh aliyepatikana na hatia
Mamlaka za Mahakama nchini Iran zimemnyonga mwanachama wa kundi la kigaidi na Kitakfiri la Daesh aliyepatikana na hatia ya kufanya mashambulizi ya kigaidi hapa nchini.
Taarifa iliyotolewa na Idara ya Mahusiano ya Umma imeeleza kuwa gaidi huyo wa Daesh amenyongwa leo asubuhi baada ya Mahakama Kuu kuidhinisha hukumu ya kifo katika kesi za kisheria. Mwanachama huyo wa Daesh aliyenyongwa ametajwa kwa jina la Mehdi Asgharzadeh.
Asgharzadeh amenyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kufanya uharibifu nchini kwa kushirikiana na kundi la kigaidi la Daesh na kuhujumu usalama wa taifa.
Rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa mtu huyo, anayejulikana zaidi kwa jina la Abu Khalid na Hussam, alipata mafunzo ya kijeshi huko Syria na Iraq, na alijaribu kutekeleza hujuma kigaidi nchini Iran.
Abu Khalid alielekea Syria baada ya kujiunga na makundi ya Kitakfiri na akapata mafunzo ya kijeshi na kiaidiolojia katika ngome kuu ya Daesh nchini humo.
Akiwa nchini Syria, Abu Khalid alisafirishwa hadi katika kambi ya Daesh katika nchi jirani ya Iraq na kupata mafunzo huko. Kisha aliingia Iran kwa siri akitokea katika eneo la Kurdistan la Iraq, akiwa pamoja na magaidi wengine watano.