Qalibaf: Muda wa kumdhibiti mbwa kichaa wa Kizayuni unayoyoma
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, Gaza ndiyo "ngome ya mwisho" ya Waislamu, na kusisitiza haja ya kuungwa mkono Palestina haraka iwezekanavyo, kabla ya ardhi nyingine katika eneo kushambuliwa na kuporwa na utawala ghasibu wa Israel.
Mohammad-Bagher Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran amezionya nchi za Kiarabu za eneo la Magharibi mwa Asia juu ya azma ya utawala wa Israel ya kujitanua zaidi katika eneo kwa kutekeleza mpango wake wa eti kuasisi "Israel Kubwa Zaidi".
Qalibaf ameyasema hayo katika ujumbe alioutuma kwa lugha ya Kiarabu kwenye mtandao wa kijamii wa X jana Ijumaa, akijibu matamshi ya hivi karibuni ya waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Akizungumza na chombo cha habari cha i24News siku ya Jumanne, Netanyahu ambaye tayari anakabiliwa na hati ya kukamatwa kwa uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya binadamu katika Ukanda wa Gaza, alifichua matarajio yake ya kutekelezwa kwa mpango unaoitwa "Israel Kubwa Zaidi". Sambamba na njama hiyo, utawala huo umeazimia kughusubu na kukalia kwa mabavu mataifa huru, ikiwa ni pamoja na Misri, Jordan, Lebanon na Syria.
Akijibu bwabwaja na ndoto hizo za alinacha za Netanyahu, Spika wa Bunge la Iran amesema katika ujumbe aliotuma kwa lugha ya Kiarabu kwenye mtandao wa kijamii wa X jana Ijumaa kuwa, "Wakati unayoyoma wa kumzuia mbwa wa Kizayuni mwenye kichaa."
Qalibaf amewahutubu viongozi wa nchi za Kiislamu kwa kuandika, "Waziri Mkuu mtenda jinai wa utawala wa Israel - Hitler huyu wa karne ya 21 - amefichua mipango ya Wazayuni kwa eneo hili kwa uwazi zaidi kuliko hapo awali.
Akiuhutubu umma wa Waislamu duniani, Spika wa Bunge la Iran amesema kuwa, Gaza ndiyo ngome ya mwisho, na kuutaka ulimwengu wa Kiislamu kuungana na kuharakisha kuisaidia Palestina kabla ya Israel kushambulia nchi nyingine.