Russia na China zasimama na Iran dhidi ya E3 kwa kutumia vibaya azimio la UN
Russia na China zimechukua hatua kukabiliana na mpango wa nchi tatu zinazounda Troika ya Ulaya, E3, na kusambaza rasimu ya azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalopendekeza "urefushaji wa kiufundi" kwa muda wa miezi sita utekelezaji wa Azimio 2231 la baraza hilo.
Rasimu hiyo iliyoandaliwa na Moscow na Beijing inatoa wito wa kusitishwa majadiliano ya kina kuhusu JCPOA hadi Aprili 2026 na inazitaka pande zote kurejea kwenye mazungumzo hayo.
Naibu Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa Dmitry Polyanskiy amesema Baraza la Usalama lazima lichague kati ya diplomasia na makabiliano.
"Njia moja inaongoza kuelekea diplomasia, amani, na mahusiano ya kawaida ya binadamu. Njia nyingine ni ya ulazimishaji na vitisho - njia iliyochaguliwa na Ufaransa, Uingereza, na Ujerumani," ameeleza mwanadiplomasia huyo.
Hayo yanajiri baada ya nchi tatu zinazounda troika ya Ulaya, yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, kwa mashauriano na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, kuijuilisha rasmi Iran kwa njia ya simu hapo jana kuhusu nia yao ya kuanzisha utaratibu wa "snapback" wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kurejesha papo kwa papo vikwazo vya baraza hilo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kutokana na mpango wake wa nyuklia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesema hatua hiyo "si ya haki, ni haramu na haina msingi wowote wa kisheria" na kusisitiza kwamba Tehran itatoa mjibizo mwafaka ili kulinda haki na maslahi yake ya kitaifa…/