Iran: Nchi za Kiislamu zinapaswa kujali zaidi kadhia ya Palestina
-
Msemaji Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa ana matumaini kwamba, nchi za Kiislamu zitafikia maelewano kwa ajili ya kulipa umuhimu mkubwa zaidi suala asili la ulimwengu wa Kiislamu yaani kadhia ya kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina.
Sadiq Hussein Jabiri Ansari amesema leo katika mkutano wa waandishi habari wa ndani na nje ya nchi mjini Tehran kwamba katika mashauriano na mazungumzo yake ya kisiasa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza udharura nchi na mataifa yote ya Waislamu kulipa umuhimu zaidi suala kuu la Waislamu yaani Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ambaye alikuwa akijibu swali kuhusu hali ya sasa ya kuwekwa kando suala hilo muhimu amesema kuwa, Iran imekuwa ikisisitiza sana umuhimu wa kutilia maanani suala la kukaliwa kwa mabavu Palestina na hatari ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaodumisha sera zake za ugaidi na kwamba nchi za Waislamu zinapaswa kuwa makini na zisiruhusu utawala huo kutumia vibaya hali ya sasa katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kuhusu mgogoro wa Syria, Jabiri Ansari amesema mgogoro huo umekuwa tata na kwamba hatua yoyote itakayochukuliwa nchini humo bila ya kushirikiana na serikali ya Damascus itatatiza zaidi hali ya mambo. Amesema inasikitisha kwamba serikali ya Saudi Arabia katika miaka ya hivi karibuni inatekeleza siasa za kuzidisha migogoro katika eneo la Mashariki ya Kati na inatumia silaha nyingi inazopewa na nchi za Magharibi kwa ajili ya kuchochea zaidi migogoro katika nchi kama Yemen na Syria. Amesema kuwa nchi hiyo inafanya mauaji ya kizazi nchini Yemen na kutumia makundi ya kigaidi katika nchi mbalimbali, suala ambalo linazidisha udharura wa kuwepo mapambano dhidi ya ugaidi.