Iran: Tunaunga mkono mpango wowote wa kumaliza vita, mauaji ya kimbari Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i131812-iran_tunaunga_mkono_mpango_wowote_wa_kumaliza_vita_mauaji_ya_kimbari_gaza
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba Jamhuri ya Kiislamu daima inaunga mkono mpango wowote unaolenga kukomesha vita na mauaji ya halaiki huko Gaza, na kusisitiza ulazima wa kuwa macho mkabala wa hulka ya utawala wa Israel ya kukiuka ahadi na makubaliano.
(last modified 2025-10-10T03:21:16+00:00 )
Oct 10, 2025 03:21 UTC
  • Iran: Tunaunga mkono mpango wowote wa kumaliza vita, mauaji ya kimbari Gaza

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba Jamhuri ya Kiislamu daima inaunga mkono mpango wowote unaolenga kukomesha vita na mauaji ya halaiki huko Gaza, na kusisitiza ulazima wa kuwa macho mkabala wa hulka ya utawala wa Israel ya kukiuka ahadi na makubaliano.

Katika taarifa iliyotolewa jana Alkhamisi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitiza uungaji mkono wa Tehran kwa hatua zinazohakikisha uondokaji wa vikosi vamizi vinavyoikalia kwa mabavu Palestina, ufikishaji wa misaada ya kibinadamu, kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina, na kurejesha haki za kimsingi za Wapalestina.

Hata hivyo wizara hiyo imeionya jamii ya kimataifa kuhusu mwelekeo hatari wa mpango huo na historia ya kutokuwa na muamana Israel.

Wizara hiyo imesema siku zote Iran imekuwa ikiunga mkono mipango inayolenga kusitisha uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza, na kuhakikisha Wapalestina wanajitawala, ikinukuu Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari wa mwaka 1948, na wajibu wa kisheria na kimaadili wa mataifa kuunga mkono mapambano halali ya Wapalestina.

Taarifa hiyo imeeleza bayana kwamba, maamuzi juu ya usitishaji vita wowote au suluhu ya kisiasa lazima yawe ya Wapalestina wenyewe, ikiwa ni pamoja na mrengo wa Muqawama.

Imesema Tehran inakaribisha uamuzi wowote unaohusu kusimamisha mauaji ya halaiki ya Wapalestina, kuondolewa kwa jeshi la Kizayuni linaloikalia kwa mabavu Gaza, kuheshimu haki ya watu wa Palestina ya kujitawala, kuruhusiwa kuingia kwa misaada ya kibinadamu Gaza na kulijenga upya eneo hilo lililozingirwa.

Haya yanajiri huku viongozi mbalimbali duniani wakiendelea kukaribisha tangazo la kusitishwa vita Gaza kufuatia siku tatu za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina ya Hamas na utawala wa kizayuni Israel nchini Misri, kulingana na mpango uliopendekezwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.