Iravani alaani mauaji ya wanadiplomasia 4 wa Iran nchini Lebanon
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameyataja mauaji ya kigaidi ya wanadiplomasia wanne wa Jamhuri ya Kiislamu katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut kama 'jinai ya kihaini'.
Katika barua yake kwa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani, Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelaani vikali mauaji hayo ya kigaidi ya wanadiplomasia wa Iran yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amesema baada ya jeshi la utawala wa Kizayuni kutishia hadharani kuwa litawalenga wanadiplomasia hao wa Iran mjini Beirut, maafisa hao walihamia kwa muda katika Hoteli ya Ramada kama hatua ya tahadhari, lakini wanajeshi wa Kizayuni wakawashambulia na kuwaua kigaidi wakiwa katika hoteli hiyo ya mjini Beirut.
Sehemu moja ya barua hiyo inasema: Mauaji ya kigaidi ya wanadiplomasia wakitekeleza majukumu yao rasmi ya kuwakilisha taifa lenye mamlaka ya kujitawala katika ardhi ya nchi nyingine huru ni kitendo cha kihaini na kigaidi, na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, ukanyagaji huo wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa na Mkataba wa 1973 wa Kuzuia na Kuadhibu Jinai Dhidi ya Watu Waliolindwa Kimataifa (wakiwemo wanadiplomasia), hautapita hivi hivi bila kujibiwa.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unabeba dhima ya jinai hiyo ya kivita dhidi ya wanadiplomasia wa Jamhuri ya Kiislamu, na unapaswa kuwajibishwa kikamilifu kwa uhaini huo.