Iran: Kuchukuliwe hatua za kimataifa kuzuia kuharibiwa Masjidul al-Aqswa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i13885-iran_kuchukuliwe_hatua_za_kimataifa_kuzuia_kuharibiwa_masjidul_al_aqswa
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kimataifa kwa ajili ya kuzuia kubomolewa msikiti mtakatifu wa al-Aqswa.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Aug 24, 2016 03:31 UTC
  • Iran: Kuchukuliwe hatua za kimataifa kuzuia kuharibiwa Masjidul al-Aqswa

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kimataifa kwa ajili ya kuzuia kubomolewa msikiti mtakatifu wa al-Aqswa.

Bahram Qassemi amesema hayo na kulaani vikali hujuma na uvamizi wa mara kwa mara wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika msikiti wa al-Aqswa na uchimbwaji wa mashimo kando kando ya msikiti huo.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuendelezwa na kufuatiliwa siasa za kuupa sura ya Uyahudi mji wa Baytul Muqaddas ni jambo lisilokubalika.

Amesema, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kimataifa kuufanya utawala ghasibu wa Israel ukomeshe hatua zake za kuuharibu msikiti wa al-Aqswa.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia pia mashambulio ya hivi karibuni ya Israel dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza na kuongeza kuwa, mashambulio haya hayajawahi kushuhudiwa kwa kiwango hiki katika miaka ya hivi karibuni.

Wanajeshi wa Israel wakiuvamia msikiti wa al-Aqswa

Amesema kuwa, mashambulio hayo yanaonyesha moyo wa kivamizi walionao maghasibu wa Quds Tukufu na hilo linathibitisha kushindwa utawala huo kukabiliana na kusimama kidete kusiko na kifani kwa wananchi wa Palestina na makundi ya mapambano.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hatua ya baadhi ya tawala ya kuwa na uhusiano na maghasibu wa Kizayuni ni sawa na kupuuza jinai zinazoendelea kila leo za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina.