Ayatullah Kermani: Wananchi wa Iran hawatasahau maafa ya Mina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i14488-ayatullah_kermani_wananchi_wa_iran_hawatasahau_maafa_ya_mina
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema kuwa, watu wa Iran kamwe hawatasahau maafa ya vifo vya kuogofya ya Mina katika msimu wa Hija mwaka jana.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 02, 2016 15:43 UTC
  • Ayatullah Kermani: Wananchi wa Iran hawatasahau maafa ya Mina

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema kuwa, watu wa Iran kamwe hawatasahau maafa ya vifo vya kuogofya ya Mina katika msimu wa Hija mwaka jana.

Ayatullah Mohammad Ali Mowahedi Kermani ameyasema hayo leo katika hotuba za Swala ya Ijumaa mjini Tehan. Ameashiria kuwadia mwezi wa Dhulhija na umuhimu wa ibada ya Hija na kusema kuwa: "Wataalamu wanasema iwapo katika ibada ya Hija mwaka jana wakuu wa Saudi Arabia wangetekeleza majukumu yao katika kudhamini usalama wa Mahujaji, basi maelfu ya Mahujaji hawangepoteza maisha katika maafa ya Mina."

Ayatullah Mowahedi Kermani amesisitiza kuwa, ibada ya Hija ni adhimu katika Uislamu na kwamba, katika kutekeleza amali za Hija, Waislamu wanapaswa kumjua adui na njama zake za kutaka kuzusha mifarakano.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran pia amebaini kuwa, iwapo Hija itatekelezwa sawa na Hija ya Nabii Ibrahim AS, basi Waislamu hawatakuwa na matatizo. Aidha ameelezea matumaini yake kuwa, Haram Mbili Takatifu zitakombolewa kutoka mikono ya Mawahabi ili Waislamu waweze kufaidika kikamilifu na ibada ya Hija sambamba na kutangaza kujibari kwao na maadui wa Uislamu.

Ayatullah Mowahedi Kermani

Ayatullah Mowahedi Kermani amewataja watawala wa Saudia kuwa ni mamluki wa Marekani na hivyo hawaruhusu Waislamu wafaidike ipasavyo na Hija.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran halikadhalika ameashiria ustawi wa Iran katika sekta ya ulinzi na kumshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kutokana na maamrisho yake ya kutaka majeshi ya Iran yajiimarishe katika kutengeneza zana za kuhujumu na kujihami.

Amesema katika dunia ambayo madola makubwa ya kibeberu na yanayotumia mabavu hayasiti kuvamia nchi zingine na kuwaua watu wasio na hatua, kuongeza uwezo wa kujihami na kuhujumu ni haki ya kimsingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullah Mowahedi Kermani amesema uwezo wa kijeshi wa Iran umepelekea maadui wa nchi hii kuingiwa na hofu na wahka..