Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu awasilisha sera jumla kuhusu kuimarisha familia
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei amewasilisha sera jumla kuhusu familia ili zitekelezwe na vyombo vyote husika nchini Iran.
Kwa mujibu wa tovuti ya ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika matini ya sera hizo jumla ambazo sasa zimetumwa kwa wakuu wa mihimili mitatu ya dola na pia kwa Mkuu wa Halmashauri ya Kuanisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu, imebainishwa kuwa, "Familia ni taasisi ya msingi katika Jamii ya Kiislamu ni kituo cha kumlea mwanadamu mwenye hadhi na ni mhimili wa afya, ustawi, nguvu na uwezo wa kimaanawi wa Iran na mfumo wa Kiislamu."
Sera hizo jumla, zimesisitiza kuhusu kuundwa jamii ambayo mhimili wake ni familia sambamba na kuimarisha familia ambayo imejengeka katika msingi wa kigezo cha Kiislamu cha familia kama kituo cha malezi ya Kiislamu. Kwa mujibu wa sera hizo jumla, familia inapaswa kuzingatiwa katika sheria, mipango, sera na katika mfumo wote wa elimu, utamaduni, uchumi na hasa katika mfumo wa ujenzi wa nyumba na miji.
Hali kadhalika katika sera hizo kumesisitizwa kuhusu kulindwa familia, kuimarisha uhusiano wa familia na misikiti sambamba na kuhifadhi na kuinua kiwango cha utambulisho wa Kiislamu na kitaifa. Katika sera hizo jumla kuhusu familia nchini Iran, nukta zingine zilizotiliwa mkazo ni kuhimiza na kurahisisha ndoa zenye mafanikio kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewasilisha sera hizo baada ya kushauriana na Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu.