Sep 07, 2016 13:24 UTC
  • Rais Rouhani:Nchi za Waislamu ziungane kukabiliana na jinai za Saudi Arabia

Rais Hassan Rouhani wa Iran ametoa wito kwa nchi za Waislamu dunaini kuungana na kuuwajibisha utawala wa Saudia kutokana na jinai zake katika nchi za Waislamu eneo la Mashariki ya Kati.

Akizungumza Jumatano mjini Tehran Rais Rouhani amesema Saudi Arabia ni muungaji mkono mkubwa wa ugaidi na imehusika katika umwagaji damu ya Waislamu wa Iraq, Syria na Yemen.

Rais Rouhani aidha amewakosoa watawala wa Saudia kutokana na uzembe na usimamizi wao mbovu katika ibada ya Hija mwaka jana ambapo maelfu ya Mahujaji wakiwemo Wairani 465 walipoteza maisha katika msongamano na mkanyagano wa wanadamu. Aidha amesema, 'serikali ya Iran na mfumo wa Kiislamu hautakubali damu za mashahidi zipotee na itachukua hatua zote za kisheria na kisiasa kutetea haki zao.'

Rais Rouhani pia amewakosoa watawala wa Saudia kwa kuweka vizingiti na kuwazuia Mahujaji Wairani kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu. Amesema Hija ni msimu wa kuleta umoja na kutetea maslahi ya Waislamu duniani lakini utawala wa Saudia haujali kuhusu hayo na hata umekataa kuwaomba radhi Waislamu kutokana na maafa ya Mina.

 

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif amesema kuwa dini ya aghalabu ya Waislamu duniani ni tafauti na Uwahhabi unaoenezwa na Wasaudi. Zarif ametoa kauli hiyo kupitia tovuti ya kijamii ya Twitter kumjibu Mfuti wa Saudi Arabia, Sheikh Abdul Aziz Al ash-Sheikh, aliyedai kuwa eti Wairani si Waislamu.

Zarif amesema hakuna uhusiano wowote baina Uislamu wa Wairani na aghalabu ya Waislamu duniani na  misimamo mikali inayohubiriwa na Mufti wa Saudia na vibaraka wake wa kigaidi.

Tags