Ayatullah Nouri Hamedani: Haram mbili tukufu ni milki ya Waislamu wote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i14950-ayatullah_nouri_hamedani_haram_mbili_tukufu_ni_milki_ya_waislamu_wote
Ayatullah Hussein Nouri Hamedani, mmoja wa Marjaa Taqlidi aliyeko katika mji wa Qom amesema: Haram mbili tukufu za Makka na Madina zilizoko nchini Saudi Arabia ni milki ya Waislamu wote duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 09, 2016 03:30 UTC
  • Ayatullah Nouri Hamedani: Haram mbili tukufu ni milki ya Waislamu wote

Ayatullah Hussein Nouri Hamedani, mmoja wa Marjaa Taqlidi aliyeko katika mji wa Qom amesema: Haram mbili tukufu za Makka na Madina zilizoko nchini Saudi Arabia ni milki ya Waislamu wote duniani.

Kiongozi huyo wa juu wa kidini ameyasema hayo alipokutana na baadhi ya familia za mahujaji wa Iran waliouawa shahidi katika maafa ya mwaka uliopita yaliyotokea katika eneo la Mina na kuongeza kuwa: "Waislamu wamekuwa siku zote wakipigiania umoja kama walivyousiwa na Qur'ani, lakini maadui wanafanya kila njia ili kuzusha mifarakano baina yao".

Alimu huyo mkubwa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ameashiria hatua ya Saudi Arabia ya kuzuia kuundwa kamati ya kutafuta ukweli ili kubaini sababu za maafa ya Mina ambapo maelfu ya mahujaji walipoteza maisha yao na kufafanua kuwa, utawala wa Aal Saud hauna ustahiki wa kusimamia maeneo matakatifu na unatumia pesa zake za mafuta  kwa ajili ya makundi ya kigaidi kama Daesh (ISIS) na kwa ajili ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mufti Mkuu wa Saudia, Abdul-Aziz ibn Abdullah Al ash-Sheikh

Ayatullah Nouri Hamedani ameeleza pia kwamba yanayofanywa na Wakufurishaji na Mawahabi yametoa pigo kubwa kwa dini ya Uislamu na kufafanua kuwa: "Matapo mawili hayo yamekuwepo kutokana na njama chafu ya wakoloni wa Magharibi na ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoukabili Ulimwengu wa Kiislamu".

Marjaa taqlidi huyo wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ameeleza pia wasiwasi alionao kutokana na kuendelea ukandamizaji wa utawala wa Aal Khalifa dhidi ya wananchi wa Bahrain na kusisitiza kuwa leo wananchi hao wanalazimika kukabiliana na utawala huo dhalimu ili kuweza kupata haki zao.../