Iran yawapongeza wanamapambano wa Palestina
-
Bahram Ghasemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewapongeza wanamapambano wa Palestina, wananchi na makundi yote ya taifa hilo kwa muqawama na kusimama kwao kidete kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mwandishi wa Radio Tehran amemnukuu Bahram Ghasemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Iran akisema hayo kwa mnasaba wa mwaka wa kwanza wa tangu kuanza Intifadha ya Quds na sambamba na kuyapongeza makundi ya wanajihadi ya Palestina, amewaenzi pia mashahidi wa Intifadha ya Quds kwa kujitolea muhanga roho zao na kusimama imara katika njia ya haki ya kupambana na wavamizi wa ardhi yao.
Amesema, hatua ya kidhulma ya Israel ya kukanyaga haki za Wapalestina, kujaribu kuugeuza kuwa wa Kizayuni mji mtakatifu wa Quds, kukivunjia heshima na kujaribu kukivunja Kibla ya Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa Al Aqsa, kupanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika adhi inazowapora Wapalesitna na kuwateka nyara, kuwatesa na kuwafunga jela wanaume, wanawake na watoto wa Palestina ni mambo yanayoikasirisha mno jamii ya kimataifa na walimwengu kiujumla.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, iwapo muqawama wa Wapalesitna utaendelea na kama taifa hilo litaendelea kushikamana na misingi yake, basi njama zote za kikatili na hila za kidhulma za utawala wa Kizayuni za kutaka kuwadhibiti kikamilifu Wapalestina, hazitafaa chochote.
Ikumbukwe kuwa siku ya Jumamosi ya tarehe Mosi Oktoba 2016 ilikuwa ni siku ya kuadhimishwa mwaka wa kwanza wa tangu kuanza Intifadha ya Quds ya wananchi wa Wapalestina ambao kwa miongo mingi sasa wamekuwa wakipambana na utawala wa Kizayuni wa Israel unaozikalia kwa mabavu ardhi zao.