Iran: Tumewanasa magaidi 11 wakijiandaa kushambulia maombolezo
Kamanda wa vikosi vya usalama nchini Iran ametangaza habari ya kutiwa mbaroni magaidi 11 katika mkoa wa Fars, kusini mwa nchi wakiwa na kilo 100 za mada za miripuko.
Ahmed Ali Gooderza amesema kuwa baada ya kupata habari juu ya uwezekano wa kutekelezwa mashambulizi na magaidi wakufurishaji katika maombolezo ya kumbukumbu ya mauaji ya Imam Hussein mjukuu wa Mtume (as), vyombo vya usalama na intelijensia viliweka mtego wa kiusalama katika maeneo yote ya mkoa wa Fars. Kwa mujibu wa kamanda wa vikosi vya usalama nchini Iran, magaidi hao walitiwa mbaroni kusini mwa mkoa huo kwa kuvamiwa ghafla na maafisa usalama wakati wakijiandaa kutekeleza shambulizi.
Katika operesheni hiyo maafisa usalama walianzisha msako ndani ya magairi na pikipiki na kufanikiwa kunasa mada za miripuko zenye uzani wa kilo 100. Kamanda Ali Gooderza ameongeza kuwa, wengi wa magaidi hao wanatoka nchi jirani.
Kwa upande wake naibu msaidizi wa masuala ya kisiasa, kiusalama na kijamii katika mkoa wa Fars Hadi Juhrumi amesema kuwa, magaidi wakufurishaji waliotiwa mbaroni walikuwa walikusudia kushambulizi marasimu ya maombolezo ya Tasua na Ashura katika Husseiniyyah na mikusanyiko ya watu.
Amefafanua kuwa, tangu mapema polisi na maafisa usalama walifuatilia harakati na nyendo zote za magaidi hao bila ya wao kujua na kuwatia mbaroni baadaye wakijiandaa kutekeleza hujuma za kigaidi. Ameongeza kuwa, baada ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kushindwa nchini Iraq na Syria, magaidi hao wamekuwa wakijaribu kupenya nchini Iran kwa lengo la kutoa pigo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.