Iran yakaribisha hatua ya UNESCO kuhusiana na Msikiti wa Al-Aqsa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekaribisha hatua ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ya kuthibitisha haki ya wananchi wa Palestina kuhusiana na ardhi na matukufu yao.
Bahram Qassimi amekaribisha azimio lililopitishwa hivi karibuni na Baraza la Utendaji la UNESCO la kukemea hatua haramu na zilizo kinyume na sheria za utawala wa Kizayuni wa Israel katika maeneo ya Palestina ukiwemo mji mtukufu wa Baitul Muqaddas na kusifu sisitizo la baraza hilo la kuthibitisha haki ya kidini ya Waislamu kuhusiana na msikiti mtukufu wa Al-Aqsa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema jibu na radiamali hasi ya utawala wa Kizayuni kwa azimio hilo ni ishara ya kukata tamaa, kuchanganyikiwa na kudhihirika hatua za hadaa za utawala huo haramu za kutaka kupotosha fikra za walimwengu na kutokubali kuwajibika kuhusiana na maazimio na sheria za kimataifa.
Katika kikao chake cha 200, Baraza la Utendaji la Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limepitisha azimio linaloeleza kuwa maeneo mawili ya Haram ya Nabii Ibrahim katika mji wa Al-Khalil na msikiti wa Bilal Ibn Rabah huko Bait- Lahm ni sehemu zisizotenganishika na ardhi ya Palestina na hazina uhusiano wowote wa kihistoria, kidini na kiutamaduni na Mayahudi.
Kufuatia kupitishiwa azimio hilo na UNESCO, Utawala wa Kizayuni wa Israel umeamua kusitisha ushirikiano wake na shirika hilo la Umoja wa Mataifa.../