Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Togo wakutana Tehran
Mawaziri wa Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Togo wamekutana leo mjini Tehran.
Katika mazungumzo hayo Mohammad Javad Zarif wa Iran na mwenzake wa Togo Robert Dussey wamejadili uimarishwaji uhusiano wa Tehran na Lome katika nyanja za kiuchumi, mapambano dhidi ya ugaidi na pia ushirikiano katika masuala ya kieneo na kimataifa. Waziri Dussey amewasili leo hapa mjini Tehran akiongoza ujumbe wa ngazi za juu.
Mapema mwezi Mei mwaka huu, Rais Hassan Rouhani wa Iran alikutana na balozi mpya wa Togo asiye mkaazi ambapo alisema Iran inalipa umuhimu mkubwa suala la kuimarisha uhusiano na nchi za Kiafrika.
Katika mazungumzo hayo Rais Rouhani alielezea matumaini yake kuwa Iran na Togo zitapanua zaidi wigo wa uhusiano wao katika nyanja za uchumi, utamaduni na siasa. Jamhuri ya Togo iko magharibi mwa Afrika na ni kati ya nchi ndogo zaidi barani Afrika.