Larijani: Uhusiano wa Iran na Russia unaridhisha mno
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema uhusiano wa pande mbili kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Russia ni wa kuridhisha mno.
Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran aliyasema hayo hapa Tehran jana Jumapili katika mkutano wake na Valentina Ivanovna Matviyenko, Mwenyekiti wa Bunge la Malodi la Russia ambaye anaongoza ujumbe wa wabunge wa nchi hiyo katika ziara ya siku mbili nchini na kuongeza kuwa, uhusiano wa kiuchumi na kiusalama wa Tehran na Moscow umeboreka na kuimarika pakubwa.
Aidha Larijani amesema wamekuwa na mazungumzo ya kufana na ofisa huyo wa ngazi za juu wa Russia, ambapo wamezungumzia vile vile suala la kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga za nishati na uchukuzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bunge la Malodi (Baraza la Shirikisho la Russia) amepongeza utekelezwaji wa makubaliano ya nyuklia ya Iran na kusema kuwa, makubaliano hayo yanayofahamika kama JCPOA yameandaa mazingira ya kuimarika zaidi uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Moscow katika nyuga za viwanda, sayansi na utamaduni.
Valentina Ivanovna Matviyenko, anatazamiwa kukutana na Rais Hassan Rouhani wa Iran na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hii Mohammad Javad Zarif, ambapo mbali na suala la uhusiano wa pande mbili, wanatazamiwa kuzungumzia mgogoro wa Syria na jinamizi la ugaidi.