Rouhani: Iran na Russia zitaendelea kupambana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i19486-rouhani_iran_na_russia_zitaendelea_kupambana_na_ugaidi
Rais wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu na Russia zitaendelea kuwa na ushirikiano wa kistratajia katika kupambana na ugaidi katika eneo hili la Mashariki ya Kati.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Nov 15, 2016 01:06 UTC
  • Rouhani: Iran na Russia zitaendelea kupambana na ugaidi

Rais wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu na Russia zitaendelea kuwa na ushirikiano wa kistratajia katika kupambana na ugaidi katika eneo hili la Mashariki ya Kati.

Rais Hassan Rouhani aliyasema hayo jana Jumatatu hapa mjini Tehran katika mkutano wake na Valentina Ivanovna Matviyenko, Mwenyekiti wa Bunge la Malodi la Russia na kubainisha kuwa, magenge ya kigaidi ni hatari sio tu kwa eneo hili bali kwa dunia yote na ili kuyasambaratisha, ushirikiano wa dhati unahitajika. Rais wa Iran amefafanua kuwa: "Ushirikiano wa Iran na Russia ni muhimu mno katika kuyatokomeza makundi hayo ya kigaidi na hususan yale yanayoendeleza harakati zao nchini Syria ili uthabiti urejee nchini humo sambamba na matakwa ya wananchi."

Wakati huo huo, kiongozi wa taifa la Iran ameongeza kuwa, Russia ni jirani muhimu wa Jamhuri ya Kiislamu na kwamba nchi mbili hizi zitaendelea kuimarisha uhusiano wao katika nyuga mbali mbali. Ameitaka Moscow na Tehran zitumie fursa ya makubaliano ya nyuklia ya Iran yajulikanayo kama JCPOA kuboresha uhusiano wa pande mbili katika nyuga za uchumi, utamaduni, sayansi na teknolijia.

Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran na Valentina Ivanovna Matvienko, Mwenyekiti wa Baraza la Shirikisho la Russia

Kwa upande wake, Valentina Ivanovna Matvienko, Mwenyekiti wa Baraza la Shirikisho la Russia amesema Tehran na Moscow zina misimamo na mitazamo inayofanana kuhusu vita dhidi ya ugaidi duniani na kusisitiza kuwa, kuna umuhimu wa kuimarishwa zaidi uhusiano wa pande mbili haswa katika uga wa nishati ya nyuklia.

Awali Mwenyekiti huyo wa Bunge la Malodi la Russia ambaye ameongoza ujumbe wa wabunge wa nchi hiyo katika ziara ya siku mbili nchini alikutana na kufanya mazungumzo na Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif.