Hamas yakadhibisha madai ya kuwepo mgogoro katika uhusiano wake na Iran
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imekadhibisha madai ya kuwepo mgogoro katika uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Afisa wa Uhusiano wa Kigeni wa Hamas, Usama Hamdan amesema uhusiano mzuri wa harakati hiyo na Iran umesimama kwenye misingi ya kuisaidia Hamas na mapambano ya watu wa Palestina na ameeleza matarajio ya kuimarishwa zaidi misaada ya Jamhuri ya Kiislamu kwa taifa la Palestina dhidi ya Wazayuni maghasibu.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, suala la kuwasaidia na kuwaunga mkono watu wa Palestina katika mapambano yao dhidi ya utawala haramu wa Israel ni miongoni mwa misingi muhimu katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Iran pia inalitambua suala hilo kuwa ni wajibu wake wa kidini na kibinadamu.
Katika upande mwingine Usama Hamdan ametilia mkazo udharura wa kuwepo mapatano ya suluhu ya kitaifa kati ya harakati na makundi mbalimbali ya Palestina na kusisitiza kwamba, ni muhimu sana kuondolewa vizuizi vyote vinavyokwamisha suala la umoja na mshikamano wa Wapalestina.