Bunge la Iran lajadili vikwazo vipya vya Marekani
Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, leo Jumapili linajadili njia za kutoa jibu kali kwa hatua ya Baraza la Seneti la Marekani ya kupitisha muswada wa kurefusha kwa muda wa miaka 10 mingine Sheria ya Vikwazo Dhidi ya Iran (ISA).
Kwa mujibu wa Alaeddin Boroujerdi Mkuu wa Kamati ya Usalama wa Kitaifa na Sera za Kigeni ya Bunge la Iran amesema bunge hilo litajadili hoja ya dharura kwa lengo la kuitaka serikali ya Iran ianze tena shughuli zote za nyuklia kwa malengo ya amani kama ilivyokuwa kabla ya mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekeelzajiwa, JCPOA baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.
Boroujerdi ameashiria hatua ya Marekani kukiuka mapatano hayo ya nyuklia na kusema kuna sheria katika bunge kuhusu ni hatua gani zichukuliwe na Iran iwapo mapatano ya nyuklia yatakiukwa. Amesema Bunge litaishurutisha serikali kutekeleza sheria hiyo.
Mkuu wa Kamati ya Usalama wa Kitaifa na Sera za Kigeni katika bunge amesema kuna umoja wa kitaifa katika kukabiliana na hatua yoyote ya Marekani kukiuka mapatano ya nyuklia.
Boroujerdi ameongeza kuwa hatua ya Bunge la Congress ya Marekani kupitisha vikwazo dhidi ya Iran imetokana na makundi ya mashinikizo ya Wazayuni na Wasaudi na kuongeza kuwa, mashirika ya Marekani ndiyo yatakayopata hasara kubwa kutokana na hatua hiyo.
Aidha amesema vikwazo vya Marekani havitakuwa na taathira kwani JCPOA si mapatano baina ya Iran na Marekani bali nchi zingine tano pia zimeyatia saini mapatano hayo.
Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani zilitia saini mapatano ya nyuklia ya JCPOA Julai mwaka jana na kuanza kuyatekeleza Januari mwaka huu.