Iran yamwita balozi wa Hungary kulalamikia vikwazo vipya vya EU
(last modified 2024-10-16T07:10:56+00:00 )
Oct 16, 2024 07:10 UTC
  • Iran yamwita balozi wa Hungary kulalamikia vikwazo vipya vya EU

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imemuita balozi wa Hungary mjini Tehran na kumkabidhi malalamiko makali ya Jamhuri ya Kiislamu kwa vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya shakhsia na taasisi kadhaa za Iran.

Giola Peto aliitwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika Masuala ya Kisiasa siku ya Jumanne. Hungary kwa sasa inashikilia urais wa kiduru wa Baraza la Umoja wa Ulaya.

Siku ya Jumatatu, Umoja wa Ulaya uliidhinisha vikwazo vipya dhidi ya shakhsia saba na mashirika saba ya Iran, ikiwa ni pamoja na shirika la ndege la Iran Air, kwa kisingizio kwamba Tehran imeipa Russia makombora ya balestiki ya kuyatumia eti katika vita vya Ukraine.

Iran imelaani hatua hiyo na kueleza kuwa, "haikubaliki" kutumia njia haramu na za kulazimisha kama vile vikwazo, ikisisitiza kwamba hatua kama hizo hazitakuwa na tija yoyote.

Mapema jana, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei alilaani hatua hiyo na kusema ni hatua isiyoweza kuhalalishika na inayokiuka sheria za kimataifa, hususan haki za binadamu.

Msemaji wa Shirika la Usafiri wa Anga la Iran (CAO) amebainisha kuwa, shirika kuu la ndege la Iran Air limesitisha safari zote za kuelekea Ulaya.

Jafar Yazarlu alisema jana Jumanne kwamba, hatua hiyo imekuja baada ya Umoja wa Ulaya kuweka vikwazo kwa mashirika ya ndege ya Iran, ikiwa ni pamoja na Iran Air, Saha Airlines na Mahan Air.

Tags