Marekani inaendelea kukiuka mapatano ya nyuklia ya Iran
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema Marekani inaendelea kukiuka mapatano ya nyuklia ya Iran na madola sita makubwa duniani.
Akizungumza Ijumaa usiku katika mahojiano na Televisheni ya Taifa ya Iran, Ali Akbar Salehi alisema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebainisha msimamo wake katika uga wa kimataifa kuhusu mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama, 'Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA."
Salehi aliongeza kuwa, nchi za Magharibi zilianza kuvunja ahadi za mapatano hayo ya nyuklia mwezi mmoja tu tangu yalipoanza kutekelezwa Januari 6 mwaka huu. Amesema benki za nchi za Magharibi zimekataa kufanya kazi na Iran hata baada ya mapatano hayo ambayo yalilenga kuondoa vikwazo dhidi ya Iran vikiwemo vya kibenki.
Kesho Jumapili, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA Yukiya Amano anatazamiwa kuitembelea Iran akiwa na ujumbe wa ngazi za juu kufuatia mwaliko wa Salehi.
Akiwa Iran atakutana na viongozi wa ngazi za juu nchini. Safari hii inajiri wakati ambao Marekani imevunja ahadi zake ilizotia saini kuzitekeleza katika mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama JCPOA.
Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani zilitia saini mapatano ya nyuklia ya JCPOA Julai mwaka jana na kuanza kuyatekeleza Januari mwaka huu.