Salehi: Iran haitavunja makubaliano ya JCPOA
(last modified Sun, 18 Dec 2016 15:17:32 GMT )
Dec 18, 2016 15:17 UTC
  • Salehi: Iran haitavunja makubaliano ya JCPOA

Mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran amesema kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitovunja makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina la JCPOA ila pale upande wa pili wa makubaliano hayo utakapofanya hivyo.

Ali Akbar Salehi amesema hayo leo Jumapili baada ya kuonana na Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) hapa mjini Tehran na kuwaambia waandishi wa habari kwamba, ripoti zilizotolewa hadi hivi sasa na wakala wa IAEA kuhusiana na miradi ya nyuklia ya Iran zinaonesha kuwa Tehran imeshikamana na kuheshimu kikamilifu na ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA.

Amesema, katika mazungumzo yake na Yukiya Amano, wamejadiliana masuala ya maji mazito ya nyuklia, urani iliyorutubishwa na utafiti na ustawishaji wa miradi ya nyuklia kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA. Amesema, Iran itaendelea kusisitiza kuwa, wajibu wa Wakala wa Kimataifa ya Nishati ya Nyuklia IAEA ni kusimamia masuala ya nyuklia duniani bila ya upendeleo na usikubali ripoti zake kuathiriwa na mtu yeyote yule.

Yuki Amano (kushoto) Mkurugenzi Mkuu wa IAEA akiwa na Ali Akbar Salehi Mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran, mjini Tehran.

 

Ikumbukwe kuwa tarehe 13 mwezi huu wa Disema, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alimpa amri mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran ya kubuni na kuunda vifaa endeshi vya nyuklia vinavyotumika katika vyombo vya usafiri wa baharini kutokana na  Marekani kupuuza, kukiuka na kuzembea kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Kwa upande wake, Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA amesema mbele ya waandishi wa habari kwamba ameridhishwa na utekelezaji wa makubaliano ya JCPOA na kwamba Iran imetekeleza ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano hayo.

Tags