Rouhani: Iran kuimarisha uhusiano wake na Niger
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtumia salamu za pongezi Rais wa Niger Mahamadou Issoufou, kwa mnasaba wa kuadhimishwa Siku ya Taifa ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Kadhalika Rais Rouhani ameliponegeza taifa hilo, kwa kuadhimisha miaka 58 ya Uhuru. Mwaka 1958, Jamhuri ya Niger ilijitangazia uhuru wake sambamba na kuzindua mfumo wa urais nchini humo.
Katika barua kwa Rais wa Niger Mahamadou Issoufou, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza matumaini yake ya kuandaliwa mazingira ya kuboreshwa uhusiano na ushirikiano wa pande mbili katika nyuga tofauti.
Aidha Rais Rouhani wa Iran ameliombea heri na fanaka taifa hilo la Kiafrika.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mara kwa mara imekuwa ikisitiza kuwa, sera zake za mambo ya nje zinatoa kipaumbele kwa kuimarishwa uhusiano na nchi za bara Afrika.