Mazoezi makubwa ya kijeshi yaanza kusini mwa Iran
Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo yanaanza mazoezi makubwa katika eneo la kusini mwa nchi.
Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Farzad Ismaili, Kamanda wa Kituo cha Ulinzi wa Anga cha Khatamul Anbiya (SAW), mazoezi hayo yatajumuisha vikosi vya Jeshi la Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC). Ameongeza kuwa luteka hiyo imepewa jina la Walinzi wa Anga za Wilayat 7 na yanaanza Jumatatu ya leo na kuendelea kwa muda wa siku tano katika eneo lenye ukubwa wa kilomita mraba 496.
Amesema mazoezi hayo pia yatajumuisha ulinzi wa mipaka ya baharini na anga ya Iran katika Bahari ya Oman, Ghuba ya Uajemi.
Brigedia Jenerali Farzad Ismaili amesema, vikosi vya Jeshi la Ulinzi wa Angani, baharini, na Nchi Kavu vya Iran vitashiriki katika mazoezi hayo.
Iran hufanya mazoezi makubwa ya kijeshi mara kwa mara ili kubaini uwezo na utayarifu wa vikosi vya ulinzi wa kuihami. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa, uwezo wake wa kijeshi si tishio kwa nchi yoyote bali sera zake za ulinzi zimejengeka katika msingi wa kujihami na kukabiliana na adui.