Iran iko tayari kushirikiana kinyuklia na nchi za eneo
Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema suala la nyuklia linaweza kuwa msingi wa ushirikiano kati ya Iran na nchi za eneo katika utumiaji wa teknolojia hiyo mpya kwa malengo ya amani.
Behruz Kamalvand amebainisha kuwa ushirikiano wa pande mbili na wa kieneo wa Iran katika uga wa nyuklia unafuatiliwa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza utayari wake juu ya suala hilo.
Kwa mujibu wa Kamalvand, hadi sasa Iran imekuwa na ushirikiano mzuri wa nyuklia na Japan, Korea Kusini, Russia na China; na kwa upande wa Ulaya na nchi za Uswisi, Poland, Hungary na Uhispania ambapo tayari imetiliana saini hati za maelewano na baadhi ya nchi au iko mbioni kufanya hivyo.
Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ameashiria pia uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kueleza kwamba ripoti za wakala huo zimethibitisha kuwa Iran imetekeleza ahadi zake…/