Saudia yaomba kufanya mazungumzo na Iran kuhusu Hija
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i22432-saudia_yaomba_kufanya_mazungumzo_na_iran_kuhusu_hija
Imedokezwa kuwa Saudi Arabia imeiomba Iran kushiriki katika mazungumzo ya kujadili suala la kuwawezesha tena Wairani kutekeleza ibada ya Hija.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 30, 2016 12:10 UTC
  • Saudia yaomba kufanya mazungumzo na Iran kuhusu Hija

Imedokezwa kuwa Saudi Arabia imeiomba Iran kushiriki katika mazungumzo ya kujadili suala la kuwawezesha tena Wairani kutekeleza ibada ya Hija.

Hatua hiyo ya Saudia inakuja baada ya nchi hiyo ya kifalme kuchukua hatua ya kuwazuia Mahujaji Wairani kushiriki katika ibada ya Hija mwaka uliopita wa Hijria.

Gazeti la al Hayat linalochapishwa London limeandika kuwa, Waziri wa Hija wa Saudia, Mohammed Bentin imeanza mazungumzo na zaidi ya nchi 80, ikiwemo Iran, kuhusu mipango ya ibada ya Hija mwaka 2017.

Gazeti hilo limeandika kuwa, 'ujumbe wa Iran umealikwa Saudia kwa ajili ya mazungumzo.'

Maafisa wa Iran hadi sasa hawajatoa tamko lolote kuhusu ripoti hiyo.

Gazeti la Arab News la Saudia pia limeandika kuwa, nchi hiyo inakaribisha mahujaji wote wakiwemo Wairani pasina kujali utaifa au madhehebu.

Maafa ya Mina, Septemba 2015

Itakumbukwa kuwa Septemba 2015, kulitokea msongamano mkubwa wa Mahujaji wakati wa ibada ya Hija huko Mina karibu na Makka. Saudia ilidai kuwa watu 770 walipoteza maisha katika msongamano huo. Hata hivyo Iran ilitangaza kuwa Mahujaji 4,700, wakiwemo Wairani 465 walipoteza maisha katika tukio hilo. Kabla ya hapo pia mahujaji wengine 100 walipoteza maisha wakiwemo Wairani 11 wakati winchi ilipoanguka katika Masjidul Haram.

Kufuatia matukio hayo, Iran ilitaka usalama wa Mahujaji udhaminiwe lakini Saudia ilikataa kushirkiana katika suala hilo na hatimaye wakuu wa Saudia wakawazuia mahujaji Wairani kutekeleza ibada ya Hija mwaka 2016.