Rouhani: Nguvu za Iran ni mwega wa usalama na uthabiti wa eneo
Rais Hassan Rouhani amesema nguvu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mwega wa usalama na uthabiti wa eneo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyasema hayo jana jioni hapa mjini Tehran katika mazungumzo na mjumbe maalumu wa Mfalme wa Kuwait na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Sheikh Sabah Khalid Al-Hamad Al-Sabah na kuongeza kwamba siasa za nje za Iran ni za kustawisha zaidi uhusiano na nchi za Kiislamu na majirani zake kwa msingi wa kuheshimiana, kuishi kwa ujirani mwema na kwa udugu wa Kiislamu.
Dakta Rouhani amebainisha kuwa japokuwa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran ilivamiwa na maadui, katika hali ambayo, yenyewe haijawahi katu kuivamia nchi yoyote, lakini imethibitisha nafasi yake ya kuwa kizuizi muhimu zaidi cha kukabiliana na uvamizi na ugaidi wa aina yoyote katika eneo.
Sambamba na kuashiria kwamba uthabiti na usalama wa eneo hasasi na nyeti la Mashariki ya Kati utapatikana kwa njia ya mazungumzo tu, na kwa urafiki na ushirikiano baina ya nchi za eneo hasa zilizo majirani, Rais wa Iran amebainisha kuwa hakuna shaka yoyote kwamba maendeleo na ustawi wa nchi na mataifa ya eneo ni kwa manufaa ya uthabiti na usalama wa wote.
Aidha amesema kwa kuzingatia fursa, uwezo na hamu ya mataifa mawili ya Iran na Kuwait, uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni wa pande mbili unapasa ufikie kiwango cha kuridhisha.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait mbali na kukabidhi ujumbe wa maandishi wa Mfalme wa nchi hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema serikali na wananchi wa Kuwait daima wanaipa heshima kubwa serikali na wananchi wa Iran na machango athirifu wa taifa hili katika eneo.
Sheikh Sabah Khalid Al-Hamad Al-Sabah aliwasili mjini Tehran jana asubuhi kwa safari ya siku moja hapa nchini.../