Jalali: Vijana kote duniani wana hamu ya kujua Uislamu halisi
Mwenyekiti wa Kundi la Urafiki wa Mabunge ya Iran na Mali amesema kuwa nchi za Waislamu zinalazimika kuarifisha sura halisi ya Uislamu kama dini ya upendo, amani na rehma kote duniani.
Kadhim Jalali ameyasema hayo katika mazungumzo yake na kiongozi wa kidini wa Waislamu wa nchi ya Mali, Sharif Othman Haidara katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bamako. Ameongeza kuwa, vijana wa Kiislamu na wasio Waislamu kote duniani wanataka kujua sura halisi ya Uislamu, kwa msingi huo wanazuoni na wasomi wa Kiislamu wana jukumu kubwa la kuarifisha Uislamu halisi.
Jalali ambaye amekwenda Mali kushiriki katika mkutano wa Jumuiya ya Mabunge ya Nchi za Kiislamu wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) amesema kuwa, misimamo ya kuchupa mipaka ni tatizo kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu na dunia nzima na kuongeza kuwa, Waislamu wanapaswa kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na ugaidi na misimamo ya kuchupa mipaka.
Kwa upande wake Sheikh Sharif Haidara ambaye ni kiongozi wa kidini wa Waislamu wa Mali amesema nchi hiyo inahisi udugu wa kidini na nchi ya Iran kutokana na misingi imara kama mafundisho ya Uislamu. Ameongeza kuwa, kuna nyanja nyingi za ushirikiano kati ya nchi hizo mbili hususan katika masuala ya dini na kukabiliana na makundi yenye misimamo mikali.