Rouhani: Iran inakaribisha kuimarika ushirikiano wake na Brazil
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i24735-rouhani_iran_inakaribisha_kuimarika_ushirikiano_wake_na_brazil
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono azma ya Brazil ya kutaka kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Tehran katika nyuga tofauti.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 05, 2017 14:24 UTC
  • Rouhani: Iran inakaribisha kuimarika ushirikiano wake na Brazil

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono azma ya Brazil ya kutaka kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Tehran katika nyuga tofauti.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo Jumapili baada ya kupokea vyeti vya Balozi mpya wa Brazil mjini Tehran, Rodrigo de Azeredo Santos na kuongeza kuwa, kuna haja ya kuimarishwa uhusiano wa kibenki kati ya nchi mbili hizi. 

Aidha Dakta Hassan Rouhani amebainisha kuwa, uhusiano wa Tehran na Brasilia umezidi kuimarika katika miaka ya hivi karibuni akisisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kupanua ushirikiano wake na Brazil katika nyuga za nishati, uchukuzi na teknolojia.

Kadhalika Rais wa Iran amefafanua kuwa, ushirikiano wa sekta binafsi za Iran na Brazil umetoa mchango mkubwa katika kuimarika uhusiano wa pande mbili katika uga wa biashara na uchumi wa nchi mbili hizi.

Kuimarika uhusiano wa kibenki kati ya Iran na Brazil

Kwa upande wake, balozi mpya wa Brazil mjini Tehran, Rodrigo de Azeredo Santos amesema kuwa, nchi yake itatumia fursa ya makubaliano ya nyuklia na kuondolewa vikwazo taifa hili, kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili katika nyuga za viwanda, kawi, uchukuzi, utamaduni, sayansi, kilimo na tenkonolojia.

Mwanadiplomasia huyo wa Brazil amesisitiza kuwa, kufikiwa makubaliano hayo ya nyuklia ya Vienna yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), kulikuwa mafanikio makubwa ya kidiplomasia, na ni muafaka ambao ulifungua ukurasa mpya kwa walimwengu kuanza kutoa kipaumbele kwa mazungumzo katika kutafutia suluhu changamoto na tofauti mbali mbali.

Aidha balozi mpya wa Brazil nchini amesisitiza kuwa, kwa sasa hakuna vizingiti vya kibenki kati ya Tehran na Brasilia, kwa kuwa serikali ya Brazil iliiagiza Benki Kuu ya nchi hiyo kushirikiana na Benki Kuu ya Iran.