Palestina; kadhia ya umoja na kipaumbele cha awali cha Ulimwengu wa Kiislamu
Msemaji wa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa kuunga Mkono Intifadha ya Palestina amesema kuwa ujumbe mkuu wa kufanyika mkutano huo hapa Tehran ni kudhihirisha suala la Palestina kama kadhia ya awali inayouhusu Ulimwengu wa Kiislamu.
Kadhim Jalali Msemaji wa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina alisema jana katika mahojiano na kanali ya pili ya Shirika la Sauti na Televisheni la Iran kuwa, kwa bahati mbaya wimbi la uchupaji mipaka, ugaidi, vita vya niaba, ukaliaji mabavu na ukandamizaji katika eneo la Mashariki ya Kati, yameiondoa kadhia ya Palestina katika vipaumbele vya awali vya Ulimwengu wa Kiislamu.
Kadhim Jalali ameshiria namna utawala wa Kizayuni unavyotumia vibaya hali ya mambo ya sasa katika eneo na kueleza kuwa, Wazayuni ndio walioanzisha machafuko na ugaidi katika eneo hili na sasa wananufaika na hali hiyo. Amesema, katika upande mwingine machafuko hayo yaliyoanzishwa na Wazayuni yanaarifishwa duniani kwa jina la Uislamu na hivyo kuzusha hofu na chuki dhidi ya Uislamu.

Msemaji wa Mkutano wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ameendelea kusema kuwa, kadhia ya Palestina ni mhimili mkuu wa umoja wa Umma wa Kiislamu na ni kwa sababu hiyo ndio maana mrengo wa uistikbari na vyombo vya habari vya Kizayuni vikafanya kila linalowezekana kuliondoa suala la Palestina katika vipaumbele vya Ulimwengu wa Kiislamu. Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina ulianza jana hapa mjini Tehran.
