Sep 28, 2024 02:15 UTC
  • Jumamosi, 28 Septemba, 2024

Leo ni Jumamosi 24 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hiijria mwafaka na 28 Septemba 2024 Miladia.

Miaka 129 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Louis Pasteur, tabibu na mwanakemia wa Kifaransa. Akiwa shuleni alisoma kwa bidii na jitihada kubwa. Baada ya kumaliza masomo yake alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika kemia na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Strasbourg huku akijihusisha uhakiki na utafiti kuhusiana na masuala mbalimbali ya kielimu. 

Louis Pasteur

 

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, alifariki dunia rais wa zamani wa Misri, Gamal Abdel Nasser. Abdel Nasser alizaliwa mwaka 1916. Alishiriki katika vita vya kwanza vya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel hapo mwaka 1948 na kufanya mapinduzi ya kijeshi kwa kushirikiana na Jenerali Najib, dhidi ya Mfalme Faruq 1952 na kuung'oa utawala wa kisultani nchini humo. Miaka miwili baadaye Gamal Abdel Nasser alimuondoa madarakani mshirika wake Jenerali Najib na kuchukua jukumu la kuiongoza Misri sanjari na kufanya juhudi za marekebisho, kupambana na ukoloni na utawala ghasibu wa Israel. Mwaka 1956 aliutaifisha mfereji wa Suez na kuufanya kuwa mali ya Misri, hatua iliyozifanya nchi za Ufaransa, Uingereza na utawala wa Kizayuni kuishambulia Misri. Hatua ya viongozi wa Misri ya kujibu hujuma hiyo, iliongeza umaarufu wa Abdel Nasser nchini Misri na ulimwenguni kwa ujumla.

Gamal Abdel Nasser.

 

Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mehr 1360 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Hujjatul Islam Sayyid Abdul Karim Hasheminejad mwanachuoni na mwanamapambano shupavu wa Iran katika mji wa Mashhad. Sayyid Hasheminejad aliuawa shahidi baada ya kupigwa risasi na mmoja wa wanachama wa kundi la Munafikiin (MKO). Mwanachuoni huyo alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi nchini Iran dhidi ya utawala wa Shah, na aliwahi kuteswa na kuwekwa gerezani mara kadhaa. 

Shahidi Hujjatul Islam Sayyid Abdul Karim Hasheminejad

 

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, makamanda 5 wa ngazi za juu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliaga dunia katika ajali ya ndege. Viongozi hao walikuwa wakirejea kutoka katika oparesheni za kuukomboa mji wa Abadan ulioko kusini magharibi mwa Iran. Mji huo wa Abadan ulikuwa umezingirwa na jeshi vamizi la dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein. Makanda hao ni Shahidi Fallahi, Shahidi Fakuri, Shahidi Namjuu, Shahidi Kolahduz na Shahidi Jahan Ara aliyekuwa kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mjini Khoram Shahr. Katika ujumbe wa kusifu na kushukuru mchango wa mashahidi hao baada ya tukio hilo Imam Khomein MA aliwataja kuwa mashahidi wa Uislamu. 

 

Katika siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio likiutaka utawala wa Kizayuni wa Israel kukomesha operesheni ya kuchimba mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Azimio hilo lililaani uchimbaji huo wa mashimo kinyume cha sheria chini ya eneo hilo takatifu. Hata hivyo upinzani wa Marekani ulipelekea kuondolewa kipengee hicho katika azimio hilo. Uchimbaji huo wa mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa na utawala huo ghasibu, ulizusha machafuko ya umwagaji damu mkubwa hapo tarehe 23 Septemba 1996 kati ya askari wa Israel na Wapalestina ambapo askari hao waliua na kujeruhi mamia ya Wapalestina.

Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

 

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita Intifadha ya wananchi wa Palestina kwa mara nyingine tena ilipamba moto. Hatua ya Ariel Sharon kiongozi wa chama chenye misimamo mikali cha Likud na mhusika mkuu wa mauaji ya halaiki ya Wapalestina katika kambi za Sabra na Shatila ya kuingia katika Msikiti wa al Aqswa na kuuvunjia heshima msikiti huo mtukufu, iliwatia hasira Wapalestina na kuwafanya waanzishe maandamano na mapambano makubwa dhidi ya utawala huo wa Israel. 

 

Tags