Iran: Jamii ya kimataifa ikomeshe mauaji ya raia nchini Yemen
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeitaka jamii ya kimataifa iingilie kati na kukomesha mara moja mauaji dhidi ya raia wasio na hatia Yemen yanayofanywa na utawala wa Saudi Arabia.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kuwa, ombwe la uongozi katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu lililosababishwa na mashambulizi ya anga ya Saudia, limeandaa mazingira ya kuenea kwa kasi harakati za kigaidi sio tu katika nchi hiyo, bali pia kieneo na kimataifa.
Taarifa hiyo imesema kuwa, uvamizi wa Aal-Saud nchini Yemen umeyumbisha usalama na amani sio tu ya nchi hiyo, bali eneo lote la Mashariki ya Kati.
Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeongeza kuwa, ni jambo la kuhuzunisha namna jamii ya kimataifa inaendelea kulifumbia macho jinai hizo dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen kila uchao.
Huku hayo yakirifiwa, wananchi wa Uingereza wamefanya maandamano katika mji mkuu London, kulaani hujuma hizo za Riyadh dhidi ya raia wa Yemen huku wakitoa wito wa kukomeshwa mashambulizi hayo, yaliyoanza Machi mwaka 2015 na ambayo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 30,000.
Mamilioni ya wananchi wa Yemen hapo jana pia waliandamana katika mji mkuu Sana'a na maeneo mengine ya nchi katika mwanzo wa mwaka wa tatu tokea Saudia ianzishe vita vyake vya kinyama dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu.