Iran, jirani mwema na mshirika mwenye utulivu na amani wa Russia
Hati 14 za ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo masuala ya kibalozi, utalii, uchumi, mawasiliano, sheria na masuala ya mahakama zimesainiwa katika mazungumzo yaliyafanyika jana kati ya Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mwenyeji wake wa Russia Vladimir Putin mjini Moscow.
Akizungumza na Rais Hassan Rouhani wa Iran, Rais Vladimir Putin wa Russia ameitaja Iran kuwa ni jirani mwema, mshirika imwenye amani na utulivu na wa kuaminika kwa nchi yake. Rais Putin ameeleza kuwa, Moscow na Tehran zinashirikiana katika nyanja zote, yakiwemo masuala ya kimataifa na katika kuyapatia ufumbuzi masuala mengi magumu na vilevile zinashirikiana katika masuala ya kiuchumi. Rais wa Russia ameongeza kuwa, ushirikiano huo si dhidi ya nchi yoyote ile.
Ziara yake Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Moscow, Russia na mazungumzo yaliyofanywa na Marais wa nchi mbili hizo yana umuhimu makhsusi. Ziara hii ya siku mbili imewaandaalia fursa viongozi wa nchi mbili hizo kuzungumzia uhusiano wa pande mbili na masuala ya kieneo na kimataifa.
Kusainiwa hati hizo za ushirikiano ni ishara ya kuimarika ushirikiano kati ya Iran na Russia. Nchi hizo mbili zimeazimia kuinua zaidi kiwango cha uhusiano wao kwa mujibu wa malengo ya kistratejia. Vilevile zimekusudia kuimarisha ushirikiano wa kiusalama katika masuala yanayohusiana na eneo hili. Aina hii ya uhusiano ina taathira muhimu katika eneo la Mashariki ya Kati na kwa sababu hiyo pi inaweza kuzusha hisia na radiamali tofauti. Radiamali hiyo inaweza kutathminiwa katika mitazamo miwili. Mtazamo wa kwanza ni ule ulioashiriwa na Rais Vladmir Putin katika mazungumzo yake na Rais wa Iran pale aliposema kuwa: Ushirikiano huo si dhidi ya nchi ya tatu.
Mtazamo mwingine ambao unakabiliana na huo ni ule wa pande ambazo hazitaki kuwepo uhusiano wa kistratejia kati ya Iran na Russia. Ni wazi kuwa duru hizo zina wasiwasi kuhusu nafasi kuu itakayokuwa nayo Iran na Russia kuhusu masuala mbalimbali ya eneo hili na zinaamini kuwa uhusiano wa aina hii utakwamisha njama za muda mrefu za Marekani katika eneo hili. Hii ni katika hali ambayo, ushirikiano uliopo kati ya Tehran na Moscow hususan katika kadhia ya Syria, umekuwa na mafanikio makubwa katika kuandaa msingi wa mazungumzo ya kisiasa ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Syria.
Pamoja na hayo yote, mitazamo ya nchi mbili za Iran na Russia haifanani katika nyanja zote, lakii wakati huo huo ushirikiano wa nchi mbili hizo katika nyanja za kiusalama umekuwa na taathira nzuri kutokana na mitazamo jumla ya nchi mbili hizo. Kwa kuzingatia uhusiano mzuri uliopo hivi sasa kati ya nchi mbili za Iran na Russia kuhusu kadhia ya Syria tunaweza kusema kwa yakini kwamba uhusiano wa Iran na Russia umeingia katika masuala ya kistratejia. Ushirikiano huo hususan katika masuala kama mkataba wa Shangai au kundi la Brix, umetayarisha uwanja wa kuwepo muungao wenye nguvu na nchi nyingine kubwa za bara Asia zikiwemo China na India. Ushirikiano huu mbali na kuwa na umuhimu katika nyanja za kisiasa, kiusalama na ushirikiano wa kijeshi kati ya Iran na Russia, una umuhimu pia katika uga wa kiuchumi.
Kwa kuzingatia nukta hiyo, Marais Rouhani na Putin wamesisitiza katika mazungumzo yao kuwa Moscow na Tehran zinashirikiana katika sekta zote yakiwemo masuala ya kimataifa na katika kuipatia ufumbuzi migogoro mikubwa na kwamba pande hizo mbili zitaimarisha zaidi ushirikiano huu.